Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Kimataifa juu ya Uhamaji (IMO) limeanzisha miradi maalumu ya kuwapatia raia wa nchi za Afrika karibu na Ghuba ya Aden mafunzo maalumu kuhusu hatari ya safari za magendo zinazokwenda kinyume na sheria. Imweripotiwa na IMO kwamba katika 2007 watu 1,400 kutokea Ethiopia na Usomali, waliochukua safari za magendo kuvuka Ghuba ya Aden walifariki ama kwa kuzama au kuuawa na majambazi waliowatorosha kimagendo. Wawakilishi wa IMO wapo Addis Ababa, Ethiopia wakijaribu kushirikiana na jumuiya za kiraia, pamoja na viongozi wa kidini kwa lengo la kuwapatia mafunzo wale wenye dhamira ya kuhama kimagendo kwenda Yemen juu ya hatari ya kuvuka Ghuba ya Aden bila ya vibali vinavyotakikana, na kuwaelezea hatari ya safari hizo na taratibu zinazotakikana kuchukuliwa kijiepusha na matatizo kama hayo katika siku zijazo.

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa litaongeza operesheni zake katika Afrika Magharibi ili kusaidia chakula cha dharura waathiriwa milioni 1.4 wa mifumko ya bei za nafaka kimataifa. Hivi sasa WFP tayari inagawa misaada ya chakula kwa watu milioni 3.6 waliopo katika Burkina Faso, Guinea, Liberia, Mauritania, Sierra Leone na Senegal. WFP itawahuduma zaidi chakula walio dhaifu, ikijumuisha watoto wadogo, wanawake waja wazito na wanaonyonyesha, na vile vile wagonjwa wa UKIMWI na VVU. Kadhalika, WFP imeamua kuweka akiba ya nafaka kwenye ghala maalumu za jumuiya, kwa madhumuni ya kuwasaidia wakulima kununua mbegu kwa bei nafuu ili baadaye waweze kuzipandisha makondeni mwao badala ya kuzila.