Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITU imeanzisha mfumo mpya kuokoa watu kwa simu ya mkononi

ITU imeanzisha mfumo mpya kuokoa watu kwa simu ya mkononi

Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU) limewasilisha utaratibu mpya wa matumizi ya simu za mkononi, uliokusudiwa kusaidia wafanyakazi wanaoshughulikia huduma za kuokoa watu kupata uwezo wa kutambua haraka nani wa kuarifiwa kwanza, kwa jamaa wa waathiriwa wa maafa au hali ya dharura. ~

Utaratibu huu utaendelezwa kimataifa na Shirika la ITU, kwa uhusiano na shirika lisio la kiserekali lijulikanalo kwa umaarufu kama 'ICE4SAFETY'. Shirika la ICE4SAFETY linahudumia mfumo wa kuwasiliana, kidharura, kwa simu za mkononi katika nchi zinazotumia lugha ya Kiingereza, ambapo orodha za majina ya watu wa kuarifiwa kidharura kwenye simu za mkononi hutumia herufi za 'ICE' kabla ya jina la mtu badala ya namba. 'ICE' ni ufupisho wa kifungu cha maneno ya Kiingereza 'in case of emergency' au kwa Kiswahili chake 'endapo kumetukia dharura'.

Lakini Shirika la ITU linaamini ni rahisi kwa nchi za ulimwengu kutumia mfumo wa aina moja, wa namba, ulio sawa, na unaotambulika kwa urahisi katika sehemu zote za ulimwengu. Kwa hivyo, ITU imapendekeza kutumiwe zile namba zijulikanazo kama rakamu za Kiarabu, kuanzia 0 mpaka 9, ambazo ni rahisi kutambulika, kuambatana na jamaa wa kuarifiwa pende tukio la dharura. Pendekezo hili la ITU litasawazisha matumizi ya kawaida, yatakayoleta natija zinazotarajiwa, bila kujali mwandiko wala lugha.