Skip to main content

Baraza la Usalama linasailia operesheni za UNAMID Darfur

Baraza la Usalama linasailia operesheni za UNAMID Darfur

Ijumatatu wajumbe wa Baraza la Usalama walionyesha kuwepo mfarakano na mgawanyika kuhusu suala la kuongeza muda wa vikosi vya mchanganyiko vya Umoja wa Mataifa/Umoja wa Afrika kwa Darfur, yaani vikosi vya UNAMID. Mataifa ya Afrika Kusini na Libya yalipendekeza kuwepo kibwagizo maalumu kwenye azimio la kuongeza muda wa operesheni za vikosi vya UNAMID, kifungu kinachoitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) kuakhirisha mashitaka dhidi ya Raisi Omar Al Bashir wa Sudan.

"Tunaamini ni muhimu sana kutia maanani masuala yenye kupewa umuhimu na Waafrika wenyewe, kudharau au kutojali maoni ya wawakilishi wa Afrika kusuluhisha matatizo yao ni kashfa na ni tusi kubwa kwa bara la Afrika.”

Alisema Balozi Mohamad operesheni za mchanganyiko za ulinzi amani za vikosi vya UM na Umoja wa Afrika katika Darfur humaanisha masuala yote muhimu yanayoambatana na mpango mzima wa kurudisha amani katika Jimbo la Darfur ni lazima yazingatiwe, kwa makini sana, na usikivu unaofaa unaowakilisha, sio UM peke yake, bali pia maoni na mawazo ya wawakilishi wa Afrika, hali kadhalika.

Shirika la Vikosi Mseto vya UM/UM kwa Darfur (UNAMID) limeripoti kwamba linaendelea kushughulikia kazi zake kikawaida katika eneo husika, na kwa sasa UNAMID inasimamia huduma za mafunzo na kuwaunganisha na Vikosi vya Wanajeshi wa Serikali ya Sudan wale wapiganaji wa zamani wa makundi ya waasi ya JEM na SLA, katika kambi za Dumaya ziliopo Nyala, Darfur. Kadhalika imeripotiwa na UNAMID kwamba katika miezi mitatu-minne iliopita watu 6,000 waliwasili kwenye kambi za wahamiaji wa ndani za Zam Zam, nje ya El Fasher, Darfur Kaskazini. Kabla ya hapo kambi ya Zam Zam ilikuwa tayari na wahamiaji 62,000 ziada.