Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Bei kubwa za chakula zaumiza malhakiri wa ulimwengu, yaonya FAO

Ripoti iliotolewa mjini Roma na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) iliozingatia matarajio ya akiba ya chakula duniani, imedhihirisha ya kuwa bei kubwa sana za chakula zilizokithiri katika soko la kimataifa sasa hivi, hudhuru zaidi walimwengu wanaoishi kwenye hali duni, umma ambao, ripoti ilitilia mkazo, hulazimika kutumia fungu kubwa la mapato yao kununua chakula.

KM azuru maeneo yaliogharikishwa na tufani Myanmar

KM Ban Ki-moon amewasili Myanmar Alkhamisi ambapo alikutana, kwa mashauriano na Waziri Mkuu, Jenerali Thein Sein na pia mawaziri wengineo ambao walisailia taratibu za kuchukuliwa kipamoja katika kuharakisha ugawaji wa misaada ya kihali kwa umma waliodhurika na janga la Kimbunga Nargis liliolivaa taifa hilo wiki tatu nyuma. Alasiri KM alipata fursa ya kuzuru eneo la Delta la Irrawaddy, na kujionea mwenyewe binafsi athari za uharibifu wa Kimbunga Nargis kieneo.

KM safarini kufuatilia huduma za dharura Myanmar

KM Ban Ki-moon amewasili Bangkok, Ijumatano na anatazamiwa kuelekea Myanmar Alkhamisi ambapo atazuru yale maeneo yaliogharikishwa na Kimbunga Nargis, na kushuhudia, binafsi, operesheni za kimataifa kuhudumia misaada ya kiutu, ya dharura, kwa waathiriwa wa tufani.

UM imewapatia waathiriwa wa zilzala Uchina fedha na mahema 11,000

UM umeifadhilia Serikali ya Uchina msaada wa dola milioni 8 kutoka ule Mfuko wa Misaada ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF. Msaada huu utakuwa miongoni mwa michango ya kimataifa iliotolewa kuwahudumia kihali waathiriwa wa zilzala iliopiga nchini huko wiki iliopita katika jimbo la kusini la Sichuan, Uchina.

Upungufu mkubwa wa chakula umetanda Ethiopia

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeonya ya kuwa taifa la Ethiopia linakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kwa sababu ya kupanda kwa bei za chakula katika soko la kimataifa, na pia kutokana na kutanda kwa ukame nchini.

Mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini yanalaaniwa na UM

Mashirika ya UM yaliopo Afrika Kusini leo yamebainisha kuingiwa wasiwasi na wahka mkuu kuhusu usalama wa wahamiaji waliopo nchini kutokea mataifa jirani, baada ya kushambuliwa katika siku za karibuni kwa sababu ya chuki za wageni. Mashambulio yalitukia na kuendelea kufanyika katika jimbo la Gauteng.