Skip to main content

Mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini yanalaaniwa na UM

Mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini yanalaaniwa na UM

Mashirika ya UM yaliopo Afrika Kusini leo yamebainisha kuingiwa wasiwasi na wahka mkuu kuhusu usalama wa wahamiaji waliopo nchini kutokea mataifa jirani, baada ya kushambuliwa katika siku za karibuni kwa sababu ya chuki za wageni. Mashambulio yalitukia na kuendelea kufanyika katika jimbo la Gauteng.

Taarifa ilisisitiza kwamba wingi wa wahamiaji wa kutoka mataifa jirani walioshambuliwa walikuwa ni watu wenye kuhishimu sheria za nchi; na baadhi yao walikuwa wanasubiri jawabu ya ombi la kupatiwa hifadhi ya kisiasa kutoka ofisi za uhamiaji. Kadhalika taarifa ya Ofisi za UM Pretoria ilisema wahamiaji waliopo Afrika Kusini lengo hasa ilikuwa ni kutafuta maisha bora kwa aila zao na walijihusisha na vibarua vya halali.

Wakuu wa Mashirika yaliopo Afrika Kusini kwenye risala yao walisisitiza kwamba wamelazimika kutoa taarifa yao kwa madhumuni ya kuongeza sauti zao za kimataifa, kupinga mashambulio ya chuki dhidi ya wahamiaji wageni. Risala ya Ofisi ya UM pia imenasihi idara za usalama Afrika Kusini, pamoja na viongozi wa jamii za huko, kuchukua hatua za haraka kuhakikisha jinai hiyo inakomeshwa, halan, na kuhakikisha walioteswa na mashambulio hayo huwa wanapatiwa hifadhi kinga inayofaa.

Mashirika ya UM Afrika Kusini yameripoti kuwa yapo tayari kupeleka misaada ya kiutu kwa wale waliodhurika na mashambulio ya wageni, na vile vile imejiandaa kujumuisha mchango wake katika kutafuta suluhu ya muda mrefu itakayosaidia kudhibiti bora tatizo la wahamiaji nchini humo.