Skip to main content

Nchi 15 zachaguliwa na Baraza Kuu kutumikia Baraza la HRC

Nchi 15 zachaguliwa na Baraza Kuu kutumikia Baraza la HRC

Ijumatano kwenye ukumbi wa Baraza Kuu,hapa Makao Makuu,wawakilishi wa Mataifa Wanachama 193 walikusanyika asubuhi kuchagua wajumbe 15 wa kuwakilishwa, kikanda, kwa kipindi cha miaka mitatu, kwenye Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu (HRC) lenye makao yake Geneva, Uswiss. ~~

Mataifa ya Chile, Brazil na Argentina yaliteuliwa kuwakilisha nchi za ukanda wa Amerika ya Latina na Karibian.

Kuhusu uwakilishi wa mataifa ya Ulaya ya Mashariki, Slovakia na Ukraine walifuzu kuchaguliwa, wakati Serbia ilitoka kapa.

Kwa upande wa nchi za Bara la Asia, mataifa yaliofuzu kugombania nafasi nne za jimbo hilo yalikuwa Ujapani, Bahrain, Jamhuri ya Korea (au Korea ya Kusini) na Pakistan. Sri Lanka na Timor Leste zilishindwa kupata kura za kutosha na kunyimwa fursa ya uwanachama wa Baraza la HRC.

Ama mapambano makali ya kura yalitukia katika kugombania viti viwili vya Ulaya ya Magharibi na Mataifa Mengine. Baada ya mvutano wa muda, Ufaransa ilifanikiwa kuchaguliwa kwa kura 123, ikifuatiwa na Uingereza ambayo ilipata kura 120, wakati Uspeni haukufanikiwa kuwa mwanachama wa Baraza la HRC baada ya kupokea kura 119.

Kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Haki za Binadamu (HRC) wanachama wake huruhusiwa kutumikia taasisi hii kwa miaka mitatu, na baada ya kutumika vipindi viwili mfululizo kwenye jopo hilo mataifa hayaruhusiwi kugombania tena uchaguzi wa Baraza la Haki za Binadamu. Wajumbe 47 wa Baraza la HRC huwakilishwa kikanda kama ifuatavyo: Bara la Afrika linawakilishwa na Mataifa Wanachama 13, Asia nao pia wana wajumbe 13, Ulaya ya Mashariki wajumbe sita, wanane huwakilisha Amerika ya Latina na Karibian na saba hujumuisha wajumbe wa nchi za Ulaya Magharibi na Mataifa Mengine.