Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Utunzaji wa viumbe anuwai unahimizwa na UM kwa natija za wote kimataifa

KM Ban Ki-moon na Raisi wa Baraza Kuu Srgjan Kerim wametoa onyo la pamoja wiki hii lenye kutahadharisha kwamba bila ya walimwengu kutunza mazingira ya viumbe na uhai anuwai, matokeo yake yatasababisha athari mbaya kimaisha, hali ambayo itaharibu na kuchafua pakubwa shughuli za uchumi, huduma za maendeleo na zile juhudi za kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa, takriban kote ulimwenguni. Onyo hili liliwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira, Achim Steiner, kwa niaba ya KM na Raisi wa Baraza Kuu kwenye mkutano wa kusailia sera za kutunza kipamoja viumbe anuwai, unaofanyika mjini Bonn, Ujerumani.

Hapa na Pale

Kwenye taarifa ya kujibu shtumu za shirika la Uingereza la \'Save the Children\' liliodai UM hauripoti udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na walinzi wa amani, dhidi ya watoto wenye umri mdogo, KM Ban Ki-moon alilazimishwa kukumbusha tena kwamba taratibu kadha za UM zimeshaingizwa kwenye kanuni zinazosimamia shughuli za taasisi hii ya kimataifa, kote duniani, kwa madhumuni ya kuhakikishia Mataifa Wanachama kwamba pindi wanajeshi, au watumishi wa kiraia wa UM watakaoshitakiwa kuendeleza kashfa hiyo dhidi ya watoto watakabili haki na watahukumiwa adhabu wanayostahiki.

Naibu Kamishna Mkuu juu ya Haki za Binadamu azuru Cote d'Ivoire na Liberia

Naibu Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Kyung-wha Kang wiki hii ameanza ziara maalumu, ya pili, katika mataifa ya Cote d\'Ivoire na Liberia ambapo atafanya mazungumzo na viongozi wenye mamlaka, makundi yanayowakilisha jumuiya za kiraia, pamoja na wanadiplomasiya, na vile vile watumishi wa vyeo vya juu wa UM na kushauriana nao kuhusu hatua za kuchukuliwa kipamoja, zitakazohakikisha kadhia ya kuhifadhi haki za raia itatumiwa kuwa ni kipengele muhimu cha upatanishi miongoni mwa makundi yanayohasimiana, na pia katika kufufua kadhia za kiuchumi na jamii kwenye mataifa husika.

Afrika yahitaji misaada maridhawa kuimarisha kilimo, NKM

Kwenye hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Siku Tatu mjini Tokyo kusailia Maendeleo katika Afrika, yaani Mkutano wa TICAD IV, Naibu KM wa UM Asha-Rose Migiro aliwahimiza wahisani wa kimataifa "kuongeza misaada maridhawa" inayohitajika kidharura kuimarisha shughuli za kilimo barani Afrika, hususan katika kipindi ambapo walimwengu wanakabiliwa na bei kubwa ya chakula katika soko la kimataifa, kitendo ambacho, alitilia mkazo NKM, kinahatarisha kuwadidimiza zaidi mamilioni ya watu Afrika kwenye fukuto la umasikini sugu.

WHO kupiga vita unywaji pombe haribifu na vileo

Kikao cha 61 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani (WHO) ambacho karibuni kilikamilisha mijadala ya wiki moja mjini Geneva, Uswiss kilifanikiwa kupitisha azimio muhimu, liliopendekeza Mataifa Wanachama kutayarisha mradi wa mwongozo utakaotumiwa katika zile juhudi za kuzuia, na kudhibiti bora matumizi haribifu ya unywaji wa vileo na pombe.

Huduma za mashirika ya UM katika Myanmar zasonga mbele

Elizabeth Byrs, Msemaji wa Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) ameripoti kutoka Geneva kwamba hivi sasa juhudi za ugawaji wa misaada ya kiutu kwa waathiriwa wa Kimbunga Nargis zimefanikiwa kuwafikia watu milioni moja katika Myanmar, wingi wao wakiwa wakaazi wa mji mkuu wa Yangon. Kadhalika, aliripoti ya kuwa watu 470,000 nao pia walipatiwa huduma za dharura na mashirika ya kimataifa, ikiwa miongoni mwa watu milioni 2 muhitaji wanaoishi kwenye miji 15 iliopata madhara makubwa ya Kimbunga Nargis.