Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Kwenye taarifa ya kujibu shtumu za shirika la Uingereza la \'Save the Children\' liliodai UM hauripoti udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na walinzi wa amani, dhidi ya watoto wenye umri mdogo, KM Ban Ki-moon alilazimishwa kukumbusha tena kwamba taratibu kadha za UM zimeshaingizwa kwenye kanuni zinazosimamia shughuli za taasisi hii ya kimataifa, kote duniani, kwa madhumuni ya kuhakikishia Mataifa Wanachama kwamba pindi wanajeshi, au watumishi wa kiraia wa UM watakaoshitakiwa kuendeleza kashfa hiyo dhidi ya watoto watakabili haki na watahukumiwa adhabu wanayostahiki.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imeripoti kwamba Jean-Piere Bemba Gombo, aliyekuwa Naibu-Raisi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, alishikwa majuzi na Serikali ya Ubelgiji baada ya kutolewa kibali cha kumkamata na Mahakama. Bemba ametuhumiwa kuongoza kundi la 'Mouvement de liberation du Congo (MLC) ambalo inasemekana lilishiriki kwenye hujuma za makosa ya vita na jinai dhidi ya utu na raia katika miaka ya 2002 na 2003 nchini Kongo.

KM Ban Ki-moon pamoja na Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour wameripotiwa kuhuzunishwa na uamuzi wa karibuni wa wenye mamlaka Myanmar ambao waliongeza tena, kwa mwaka wa sita, kifungo cha nyumbani dhidi ya Daw Aung San Suu Kyi, Katibu Mkuu wa chama cha Umoja wa Demokrasia ya Taifa (NLD).

Baraza la Usalama lilikutana Ijumatano kwenye kikao cha hadhara kuzingatia hali Mashariki ya Kati ambapo Robert Serry, Mshauri Maalumu juu ya Mpango wa Amani katika Mashariki ya Kati aliwaambia wajumbe wa Baraza kwamba anaunga mkono mafanikio yaliojiri karibuni Lebanon, na pia mazungumzo ya faragha kati ya Israel na Syria; lakini hata hivyo, alihadharisha, amani ya jumla haitopatikana Mashariki ya Kati bila ya, kwanza, kuondosha vile vizingiti kadha wa kadha sugu vilivyojizatiti kieneo.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour ameripoti kushutushwa sana na taarifa alizopokea juu ya kugunduliwa maiti kadha za wanaharakati wa kisiasa waliouawa Zimbabwe, na alishtumu vikali pia mauaji na unyanyasaji wa wafanyakazi wa mashirika yasio ya kiserekali, pamoja na wale wanaharakati wanaohudumia haki za binadamu na wanachama wengine wa jumuiya za kiraia yanayoendelezwa Zimbabwe.

[na mwishowe] Ujumbe maalumu wa Baraza la Usalama unatarajiwa kuondoka New York Ijumamosi kuanza ziara ya siku 10 barani Afrika, kusailia hali ya usalama na amani na miongni mwa nchi ambazo tume itazuru inajumuisha Djibouti ambapo mazungumzo ya upatanishi wa Usomali yanaendelezwa; na vile vile watakwenda Sudan, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Cote d'Ivoire.