Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Bangkok unajadilia udhibiti mpya wa mabadiliko ya hali ya hewa

Mkutano wa Bangkok unajadilia udhibiti mpya wa mabadiliko ya hali ya hewa

Ijumatatu, wajumbe wanaokadiriwa 1,200 kutoka Mataifa Wanachama 160 ziada walijumuika mjini Bangkok, Thailand kuanza duru ya kwanza ya mazungumzo ya siku tano, yanayoungwa mkono na UM, kuzingatia na kusailia mapatano mapya ya kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Hotuba ya ufunguzi ya KM wa UM, Ban Ki-moon kwa njia ya vidio, ilizihimiza nchi zote kusirikiana kutafuta suluhu ya kuridhisha juu ya suala la mabadiliko ya hali ya hewa, suluhu ambayo umma wa kimataifa wataweza kuimudu kiuchumi na yenye "msingi wa maadili yenye kutilia mkazo dhamana na majukumu tofauti" yenye natija kwa umma wote wa kimataifa.

Matumizi halali ya kanuni za Mkataba wa Kyoto yanatarajiwa kumalizika katika 2012, na ni matarajio ya UM mkataba mpya utapatiwa fursa ya kuzingatiwa kwenye bunge za nchi wanachama mapema zaidi, ili uidhinishwe na kuridhiwa Mkataba wa Kyoto kumalizika.