Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Walinzi wa Amani Duniani

Tangu miaka mitano iliopita, UM uliweka kando tarehe 29 Mei kuwa ni siku ya kuadhimishwa rasmi mchango wa wafanyakazi wa kimataifa, waume na wake, wa kutoka kanda mbalimbali za dunia ambao walitumia ujuzi wao, chini ya bendera ya UM, kulinda na kuimarisha amani ya kimataifa, na kuwapunguzia mateso ya hali duni umma wa kimataifa, pamoja na kuendeleza haki za binadamu na kudumisha huduma za maendeleo katika sehemu kadha wa kadha za ulimwengu.

UM walaani vikali ukatili na mauaji karaha yaliotukia DRC Mashariki

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kutukia karibuni katika vijiji vya Nyabuluze na Mhungu, Kivu ya Kusini mashambulio yasiochokozwa, ambapo raia 19 waliuawa, wakiwemo watoto wadogo na wanawake. Wanamgambo wa Rasta pamoja na waasi wa kundi la Rwanda linaloitwa FDLR ndio wanaotuhumiwa kuendeleza vitendo hivi vilivyoharamisha mipaka ya kiutu.

Majambazi wavamia malori ya WFP Uganda

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kwamba majambazi fulani walishambulia, kwa kuvizia, msafara wa malori ya UM katika jimbo la Karamoja la Uganda kaskazini-mashariki na kumwua dereva, Richard Achuka, 41, tukio ambalo limeilazimisha WFP kusitisha kwa muda operesheni za kuhudumia waathiriwa wa ukame nusu milioni chakula kwenye eneo husika.

Mashirika ya UM yajumuika kukomesha utapiamlo Ethiopia

Shirika la WFP pamoja na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) yamenuia kuisaidia Ethiopia kukabili tatizo la kuviza na kudumaza kwa watoto, tatizo ambalo huchochewa na ukosefu wa lishe bora katika mwili. Mradi huo unatazamiwa kufadhiliwa kutoka msaada wa Kamisheni ya Ulaya (EC) ambayo itajumuika na WFP na UNICEF pamoja na Serekali ya Ethiopia kusaidia wale mama na watoto waliokabiliwa na hali duni kupata huduma za kuboresha lishe na, hatimaye, kuwaepusha vijana na tatizo la kudumaa na kukua na kimo kidogo.

UM kusaidia wanasiasa Sierra Leone kupata welekevu wa vyombo vya habari

Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) pamoja na Ofisi ya Kufufua Kadhia za Uchumi na Jamii Sierra Leone (UNIOSIL) yamefanyisha warsha maalumu kwenye mji mkuu wa Freetown, Sierra Leone kuwasaidia wawakilishi wa vyama vya kisiasa kupatiwa uzoefu na welekevu juu ya mbinu za kuwasiliana na umma kwa kueneza ujumbe unaoambatana na itikadi zao za kisiasa, kwa kutumia vyombo vya habari.

Hapa na pale

Jamii ya Kundi la Washauri wa UM juu ya Huduma za Fedha imetangaza taratibu mpya kadha za kuhamasisha jumuia mbalimbali - ikijumuisha serekali, wahudumia maendeleo na pia sekta ya binafsi - kuwasaidia watu masikini, hususan katika mataifa yanayoendelea, kupata fursa ya kushiriki kwenye huduma za fedha, mathalan, uwezo wa kufungua akaunti ya benki, kuchukua mikopo, au kununua bima, huduma ambazo zikitekelezwa zitausaidia umma masikini kuwekeza fedha hizo kuboresha maendeleo katika sekta za uchumi na jamii.