Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali katika Chad na Maziwa Makuu ilizingatiwa na Baraza la Usalama

Hali katika Chad na Maziwa Makuu ilizingatiwa na Baraza la Usalama

Dimitri Titov, mkurugenzi wa kitengo kinachohusika na masuala ya Afrika cha Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za UM (DPKO) majuzi alikuwa na mashauriano ya faragha na wajumbe wa Baraza, kuzingatia matokeo ya ukaguzi wa ziara ya ujumbe wa UM katika Chad kuhusu hali ya usalama, kwa ujumla, katika nchi.

Kadhalika, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour alikutana na wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye kikao cha faragha, ambapo alielezea juu ya ziara yake ya hivi karibuni kwenye Eneo la Maziwa Makuu, ikijumuisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Burundi. Baadaye Arbour alikutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu ya UM, na aliwaambia kuwa amekirihishwa sana na ripoti alizopokea kuhusu jinai iliofanyika katika eneo la Maziwa Makuu ambapo watu walinajisiwa kihorera, hususan katika Burundi na DRC. Kadhalika, Arbour alishtumu makosa ya udhalilishaji wa kijinsia, vitimbi ambavyo vilikiuka haki za kimsingi. Arbour alihadharisha ya kuwa ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuchukua kila hatua ya kisheria, kuhakikisha wakosa wa jinai ya kijinsia watashikwa na watafikishwa mahakamani.