Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Jamii ya Kundi la Washauri wa UM juu ya Huduma za Fedha imetangaza taratibu mpya kadha za kuhamasisha jumuia mbalimbali - ikijumuisha serekali, wahudumia maendeleo na pia sekta ya binafsi - kuwasaidia watu masikini, hususan katika mataifa yanayoendelea, kupata fursa ya kushiriki kwenye huduma za fedha, mathalan, uwezo wa kufungua akaunti ya benki, kuchukua mikopo, au kununua bima, huduma ambazo zikitekelezwa zitausaidia umma masikini kuwekeza fedha hizo kuboresha maendeleo katika sekta za uchumi na jamii.

Ripoti ya nusu mwaka ya Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (DESA) kuhusu Hali na Matarajio ya Uchumi Duniani kwa 2007 imehadharisha ya kuwa uchumi wa kimataifa, kwa ujumla, utazorota na kupwelewa kimaendeleo pindi jamii ya kimataifa itaruhusu thamani ya dola kuporomoka kwa kasi, na imetilia mkazo umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka kipamoja kudhibiti bora hali hiyo.

Wabuni sera za maendeleo, wataalamu wa soko la nafaka pamoja na wanauchumi wa kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekutana kwenye mji wa Roma, Utaliana katika mkutano muhimu uliotayarishwa na WFP kuzingatia njia bora ya kuwanufaisha wakulima wa mataifa yanayoendelea kwa kununua chakula kutoka wakulima hao katika zile nchi ambazo huwa zinapokea misaada ya chakula katika nchi zinazoendelea badala ya kuagizishia kutoka nchi za kigeni.

Martin Scheinin, Mkariri Maalumu wa UM anayesimamia utekelezaji wa haki za binadamu na hifadhi ya haki za kimsingi kwenye mazingira vita dhidi ya ugaidi, amewakilisha ripoti kuhusu ziara ya siku kumi aliofanya Marekani hivi majuzi na amesisitiza kutokubaliana na uamuzi wa serekali ya taifa hilo wa kuwaweka vizuizini kwenye magereza ya Ghuba ya Guantanamo, Cuba na katika jela za Iraq, Afghanistan pamoja na kwenye maeneo mengineyo ya siri wale watu waliotuhumiwa kushiriki kwenye ugaidi, bila ya hukumu ya kesi, na vile vile ameshtumu matumizi ya “mbinu za kisasa za kusaili kutafuta ushahidi” na amepinga, halkadhalika, matumizi ya mahakama za kijeshi kuhukumu mateka hao.

[na hatimaye]

KM Ban Ki-moon amemteua Francis Deng wa Sudan kuwa Mshauri Maalumu wake juu ya Huduma Kinga dhidi ya Mauaji ya Halaiki na Ukatili wa Umma.