Mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaanza mwezi huu wa Septemba hadi wiki ya pili ya mwezi Septemba mwakani. Katika ukurasa huu hata hivyo tutakuwa tunakuletea habari motomoto kutoka mjadala wa wazi na vikao vya ngazi ya juu vya mkutano huo ambavyo vinafanyika kuanzia tarehe 25 septemba 2018 hadi Oktoba mosi 2018. Pamoja na hotuba za viongozi ni vikao vya ngazi ya juu kuhusu Kifua Kikuu, Ulinzi wa Amani, tukio maalum la kumuenzi hayati Nelson Mandela na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs.
MKUTANO WA 73 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Chonde chonde Umoja wa Mataifa tuondoleeni vikwazo vya silaha:Somalia
Ninausihi Umoja wa Mataifa kuiondolea Somalia vikwazo vya ununuzi wa silaha . Wito huo umetolewa leo na Ahmed Isse Awad Waziri wa mambo ya nje wa Somalia akihutubia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 mjini New York Marekani hii leo.
Wanahabari 262 wamefungwa mwaka jana pekee, hii si haki:UN
Waandishi wa mara kwa mara hutishwa, hushambuliwa na hata kuuawa, na idadi kubwa wanafungwa gerezani duniani kote. Hayo yameelezwa bayana na wataalamu wa haki za binadamu kwenye mkutano uliofanyika kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York Marekani.
Sasa Burundi tuna amani na wakimbizi wanarejea nyumbani:Nibigira
Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Ezechiel Nibigira ameuambia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 unaoendelea mjini New York Marekani kuwa hivi sasa taifa lake lina utulivu na amani na wakimbizi walioko nje wameanza kurejea nyumbani, hivyo ni wakati wa Baraza la Usalama kuacha kulijadili taifa hilo kila uchao.
Kwa ujumla usalama umerejea Burundi na wakimbizi wanarudi: Nibigira
Waziri wa mambo ya nje wa Burundi amesema kwa ujumla hali ya usalama na utulivu imerejea Burundi na kilichosalia ni matukio madogomadogo ya utovu wa nidhamu.
Vita vyetu dhidi ya ugaidi vinakaribia ukingoni: Syria
Naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Muallem amesema vita vya nchi yake dhidi ya ugaidi vinaelekea ukingoni akishukuru ujasiri, dhamira, umoja wa watu wa Syria, jeshi la nchi hiyo, msaada wa marafiki na washirika wao.
Mshikamano ndio suluhu pekee ya maendeleo duniani:Chad
Ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwa wote duniani , hakuna chaguo lolote la kufikia azma hiyo isipokuwa kufanya kazi pamoja , kuibua vitosho vilivyopo na kukabiliana na changamoto zinazoughubika ulimwengu kwa kuzingatia misingi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.