Skip to main content

Sudan Kusini ya mwaka jana si ya mwaka huu, shukrani UN, AU na wadau- Gai

Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani
UN /Kim Haughton
Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani

Sudan Kusini ya mwaka jana si ya mwaka huu, shukrani UN, AU na wadau- Gai

Amani na Usalama

Mwaka jana nilisimama mbele yenu nikiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi iliyogubikwa na vita. Leo hii nimesimama tena mbele yenu kama shuhuda wa kile ambacho wanachama wa chombo hiki adhimu wamesaidia kufanikisha ndani  ya Jamhuri ya Sudan Kusini.

Ni kauli ya Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini aliyotoa wakati akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Akiwa anamwakilisha Rais Salva Kiir ambaye amesema ameshindwa kuhudhuria kutokana na majukumu ya kuimarisha amani nchini mwake, Bwana Gai amesema, “Napenda kujulisha chumba hiki adhimu kuhusu Sudan Kusini iliyounganika zaidi, ambayo inaelekea kwenye amani na utulivu. Kutokana na kuendelea kwa usaidizi na nia njema kutoka kwa wadau wa kimataifa na kikanda tuko katika ratiba yetu ya kufanya uchaguzi mkuu huru na wa haki baada ya kipindi cha mpito cha miezi 36.”

Amesema kutiwa saini kwa azimio la Khartoun la makubaliano kati ya pande kinzani nchini Sudan Kusini tarehe 27 mwezi Juni mwaka huu kati ya Rais Kiir na makamu wake wa zamani wa Rais, Riek Machar na viongozi wengine wa kisiasa, pande hizo zimerithia sitisho la kudumu la mapigano Sudan Kusini na pia kupitisha makubaliano kuhusu masuala ya ulinzi ili kujenga jeshi, polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vya kitaifa.

Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018

Bwana Gai amesema pamoja na mkataba mwingine ulioboreshwa ambao ulitiwa saini hivi karibuni kati ya Rais Kiir na Bwana Machar, Sudan, “Tumeanza pia mjadala wa kitaifa na mpango wa raia wa mashinani tangu disemba mwaka 2015. Ni imani  yetu kuwa mfumo huu w apande tatu utaimarisha juhudi za amani mashinani,”

Mchakato  huu  umetoa fursa kwa wale ambao hawakuwa na fursa ya kupaza sauti zao ili zisikike, na hivyo kuanza kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali.

Makamu huyo wa kwanza wa Rais nchini Sudan Kusini ameendelea kupigia chepuo mpango huo wa mashinani akisema kuwa umekuwa na ufanisi ambapo wajumbe wa kamati husika wanatembelea mikoa kuanzia ngazi ya chini kuhoji maswali yenye lengo la kubaini chanzo cha mgawanyiko na wakati huo huo mapendekezo ya suluhisho na kuweka maridhiano, “Mchakato  huu  umetoa fursa kwa wale ambao hawakuwa na fursa ya kupaza sauti zao ili zisikike, na hivyo kuanza kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali. Ripoti kutoka mashinani zilikuwa ni nzuri mno na wanachi waliruhusiwa kutoa maoni yao bila woga wala hofu ya kukumbwa na visasi. Tunasubiri kwa hamu kuona hatua zinazofuata wakati huu ambao tunaingia kipindi cha mpito.”

Makamu huyo wa Rais ameshukuru taasisi za kikanda ikiwemo IGAD, AU pamoja na zile za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa kwa jinsi ambavyo zimekuwa bega kwa bega na Sudan Kusini kuhakikisha mzozo ulioanza mwezi disemba mwaka 2013 unafikia ukomo na amani ya kudumu inapatikana kwa taifa hilo changa zaidi duniani.