"Amani na usalama wa dunia uko mikononi mwetu viongozi"- Rais Masisi wa Botswana

27 Septemba 2018

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York, Marekani, amezitaka pande zote zilizoko katika migogoro kote duniani kufikiria juu ya wananchi wao na kuhakikisha zinawajibika kuwalinda kwa mujibu wa haki na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Akizitaja nchi kama Afghanstan, Mali, Sudani Kusini, Syria na Yemen Rais Masisi amefafanua zaidi kuwa vurugu zinazosababishwa na kutokuelewana kote duniani zimesababisha zaidi ya watu milioni 68.5 kuyahama makazi yao.

“Utafiti unaonyesha kuwa mogogoro inachangia ongezeko la makazi duni na baa la njaa na hivyo kuzidi kukomaza janga kwa wanadamu” amesema rais  Masisi.

Amesema pia ili kutunza amani na usalama duniani, migogoro yote imalizwe kwa njia ya mazungumzo na makubaliano ya amani.

Rais Masisi pia amempongeza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa kuhamasisha mabadiliko ndani ya Umoja wa Mataifa yanayolenga kuimarisha uwezo wa umoja huo katika kuzuia migogoro na vilevile kutafuta suluhu, mazungumzo ya amani, kulinda amani, ujenzi na uendelezaji baada ya maigogoro, ukuzaji na uendelezaji wa amani.

Aidha rais huyo mpya wa Botswana aliyepokea kijiti kutoka kwa Rais Dkt. Seretse Khama Ian Khama mapema mwaka huu, akapongeza kuhusiana na namna viongozi wa Afrika walivyojizatiti kuwezesha kifedha asilimia 25 ya operesheni za amani barani Afrika kufikia mwaka 2021 na kunyamazisha bunduki ifikapo mwaka 2020, akisema kuwa hali hiyo itasaidia kuondoa changamoto za kiusalama hasa katika eneo la Afrika ya kati na Magharibi hususani vitisho vya ugaidi kule ziwa Chad na eneo la Sahel-Sahara.

“Ninazipongeza nchi wanachama wa Jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika ya Kati ECCAS na Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS kwa kuyachukua makubaliano ya Lomé Togo kuhusu amani, usalama,na mapambano dhidi ya ugaidi” amesema rais Mokgweetsi Masisi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter