Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa kuna nuru kwa Sudan na Sudan Kusini kumaliza tofauti zao- Waziri Eldirdiri

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Eldirdiri Mohamed akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Eldirdiri Mohamed akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Sasa kuna nuru kwa Sudan na Sudan Kusini kumaliza tofauti zao- Waziri Eldirdiri

Amani na Usalama

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohamed Ahmed Eldirdiri amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa mazingira ya sasa yanatia moyo katika kupatia suluhu masuala yote yaliyosalia kati ya  nchi yake na Sudan Kusini.

Dkt. Eldirdiri amesema juhudi za usuluhishi zinazofanywa na Rais wa Sudan Omar Al Bashiri na pande za Sudan Kusini zimefungua awamu mpya kati ya nchi hizo.

Amesema hatua ya sasa isingalikuwa ya mafanikio bila ya kitendo cha imani kwa Rais Bashir kutoka kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani Dkt. Riak Machar.

Dkt. Eldirdiri amesema “ nawaeleza wale wote wenye shaka kuhusu uwezo wa viongozi wa Sudan Kusini kufanya kazi kwa pamoja au shaka kuhusu nia yao au uwezo wa mataifa ya ukanda huo kuendelea kuungana na Sudan Kusini, kuwa hivi sasa hakuna njia zaidi ya kuipatia fursa amani.”

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema hakuna matumaini wala nuru kwa Sudan  Kusini na ukanda mzima bila kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya pande kinzani nchini Sudan Kusini.

Dkt. Eldirdiri amesema kutokana na njia ya matumaini kufunguka Sudan Kusini, hivi sasa nchi mbili hizo tayari zimeanza mashauriano yasiyo rasmi, mashauriano ambayo yanaweza kuimarisha kuaminiana na kuondokana kabisa na  ukurasa wa kutokukubaliana.