Waliohutubia UNGA73: Marais 77, wakuu 44 wa serikali, mawaziri 54, naibu mawaziri wakuu 4, Naibu Waziri 1, wawakilishi 8 wa kudumu wa nchi kwenye Umoja wa Mataifa.
Mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umekunja jamvi hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo Rais wa baraza hilo Maria Fernanda Espinosa amesema umekuwa na mafanikio makubwa hususan kutiliwa mkazo suala la ushirikiano wa kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, kutoa tathmini ya mkutano huo ulioanza tarehe 25 mwezi Septemba na kumalizika leo tarehe Mosi Oktoba, Bi. Espinosa amesema suala la ushirikiano wa kimataifa ni mojawapo ya vipaumbele vyake saba ambavyo anavitilia maanani.
Vipaumbele vingine ni usawa wa kijinsia, uhamiaji na wakimbizi, kazi yenye utu, watu wenye ulemavu, hatua dhidi ya mazingira, vijana na amani na usalama pamoja na kuhuisha Umoja wa Mataifa.
Kwa mantiki hiyo amesema “nimeazimia kushirikiana na nchi zote wanachama kwenye ukumbi huu ili kuhakikisha utekelezaji wa vipaumbele hivi unakuwa na tija, unakwenda bila tafrani na uwe ni mwaka wa kupata matokeo ya kina kwa watu wote tunaowahudumia duniani.”
Ametaja mafanikio mengine ni kupitishwa kwa azimio la kisiasa juu ya kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB sambamba na lingine la kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs.
Bi. Espinosa amepongeza marais, viongozi na mawaziri kutoka nchi kadhaa waliohusika na maandalizi ya maazimio hayo akisema kilichobakia sasa ni kutekeleza kilichomo kwenye maazimio hayo yanayolenga kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jumla ya marais 77 marais walihudhuria bila kusahau wakuu 44 wa serikali, mawaziri 54, naibu mawaziri wakuu 4, Naibu Waziri 1 na wawakilishi 8 wa kudumu wa nchi kwenye Umoja wa Mataifa.
Amezungumzia pia urefu na ufupi wa hotuba akisema ndefu zaidi ilitolewa na Venezuela kwa dakika 48 ilhali Lithuania walivunja rekodi kwa kuwa na hotuba iliyodumu kwa chini ya dakika 5.