Tunaunga mkono ushirikiano wa kimataifa- Tanzania

27 Septemba 2018

Tanzania imetaka hatua za dhati zichukuliwe ili kuokoa hoja ya  ushirikiano wa kimataifa ambao hivi sasa uko mashakani.

UHUSIANO WA KIMATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Balozi Augustine Mahiga amesema hayo wakati akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani wakati huu ambapo kuna vuta nikuvute kuhusu mustakhbali wa ushirikiano wa kimataifa.

Baadhi ya nchi zinataka kuondokana na mpango huo ilihali zingine ikiwemo Tanzania ikitetea ikisema kuwa ndio muarobaini wa changamoto zinazokumba dunia hivi sasa.

Balozi Mahiga akifafanua msisitizo wa ushirikiano wa kimataifa amesema “ hii leo tunaishi katika dunia ambamo kwayo jamii nyingi hazina amani, hazina usawa na si endelevu. Dunia bado inakumbwa na mapigano na vita vinavyosababisha vifo vya binadamu, tishio la ugaidi, uharibifu wa mazingira, wimbi la wakimbizi, njaa na umaskini. Kushughulikia changamoto hizi kunahitaji mshikamano wa pamoja.”

SABABU YA KUMWAKILISHA RAIS JOHN MAGUFULI

aziri huyo wa Mambo ya Nje wa Tanzania ambaye amemwakilisha Rais John Magufuli alitaja sababu ya Dkt. Magufuli kushindwa kuhudhuria mkutano huo kuwa ni ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere mwezi huu wa Septemba huo mkoani Mwanza, na kusababisha vifo vya watu zaidi y a 200 na wengine kujeruhiwa. Akatumia fursa hiyo kusema, “tunashukuru msaada wenu na jamii ya kimataifa wakati huu wa kipindi kigumu.

WAKIMBIZI

Suala la wakimbizi wa Burundi nalo pia limezungumziwa na Balozi Mahiga akisema mchakato wa wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari umekumbwa na mkwamo kutokana na ukosefu wa rasilimali. Hivyo ameomba jamii ya kimataifa isaidie ili zoezi hilo liweze kuendelea licha ya uzushi uliotolewa na baadhi ya wakimbizi waliopatiwa hifadhi ya kisiasa nje ya nchi ya kwamba zoezi hilo si la hiyari.

MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU, SDGS

Amezungumzia pia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambapo Waziri huyo wa Mambo ya Nje amesema kutokana na kile walichojifunza wakati wa utekelezaji wa malengo ya milenia, sasa Tanzania imejumuisha  SDGs katika ajenda yake ya maendeleo ya kitaifa.

Hata hivyo amesema wamegundua kuwa “uhamasishaji wa kipindi kirefu wa fedha kutoka sekta ya umma na ile ya binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo hayo ambayo ukomo wake ni mwaka 2030.”

ULINZI WA AMANI

Ulinzi wa amani ambao ni moja ya shughuli za Umoja wa Mataifa ambazo Tanzania inashiriki, ulipatiwa nafasi katika hotuba ya Balozi Mahiga ambaye amesema “tunapongeza hatua zilizochukuliwa kufuatia kisa cha Beni mwezi Disemba mwaka jana ambapo Katibu Mkuu aliunda jopo la uchunguzi na mapendekezo yakatolewa. Tunatumia yatatekelezwa.” 

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO, DRC

Balozi Mahiga akazungumzia hali ya amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC akisema kuwa madhila yanakumba raia kila uchao wakati huu ambapo uchaguzi ulioahirishwa mara kadhaa unasubiriwa kwa hamu. “Utulivu nchini DRC hauleti unafuu kwenye suala la wakimbizi pekee, bali pia unachagiza biashara ya kikanda na kushamiri kwa fursa za kiuchumi.”

Hakuwezi kuwepo na hakikisho bora zaidi kuhusu mustakhbali na maendeleo na hali ya kisiasa nchini DRC kuliko tamko lililotolewa kutoka mimbari hii na mheshimiwa Rais Joseph Kabila siku chache zilizopita

Kwa mantiki hiyo balozi Mahiga amesihi jamii ya kimataifa iipatie DRC msaada wa vifaa na fedha ili iweze kukamilisha maandalizi ya uchaguzi na kufanyika uchaguzi wenyewe.

“Hakuwezi kuwepo na hakikisho bora zaidi kuhusu mustakhbali na maendeleo na hali ya kisiasa nchini DRC kuliko tamko lililotolewa kutoka mimbari hii na mheshimiwa Rais Joseph Kabila siku chache zilizopita,” amesema Waziri Mahiga.

Kwa mantiki hiyo amesema “ni muhimu kuacha ujumbe wa kulinda amani nchini humo MONUSCO pamoja na kikosi cha kujibu mashambulizi, FBI viendelee kuwepo DRC hadi baada ya uchaguzi uliopangwa kufanywa baadaye mwaka huu.

TANZANIA NA UMOJA WA MATAIFA

Hata hivyo zaidi ya yote amerejelea ahadi ya Tanzania ya kuzingatia misingi na malengo ya Umoja wa Mataifa na ushirikiano wa  kimataifa akisema kuwa “Tanzania iko tayari wakati wowote kushiriki kwa ufanisi katika kusaka suluhu za mzozo kwa njia ya amani na kuchangia katika operesheni za Umoja wa Mataifa za kuzuia mizozo na pia kulinda amani.”
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter