Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugaidi unaoendelea sasa hauhusiani na dini: Libya.

Mohamed Siala,  waziri wa mashauri ya kigeni wa Libya, akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 28 Septemba 2018
UN Photo/Loey Felipe
Mohamed Siala, waziri wa mashauri ya kigeni wa Libya, akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 28 Septemba 2018

Ugaidi unaoendelea sasa hauhusiani na dini: Libya.

Masuala ya UM

Serikali ya Libya imesema inalaani ugaidi wa aina yoyote ile bila kujali umefanywa na nani na kwa misingi gani.

Akihutubia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York Marekani , Bw Mohamed Siala, waziri wa mashauri ya kigeni wa Libya  amesema ugaidi ni changamoto inayoikumba dunia nzima na haunamshikamano na  dini yoyote.

Ameongeza kuwa taifa lake limejitolea kuendesha vita dhidi ya makundi ya kigaidi yaliyo na wapiganaji wa kigeni kama vile Daesh ambao waliingia Libya kutoka nje ajambo ambalo amesema si tisho tu kwa usalama wa Libya lakini pia kundi hilo linapora maliasili ya nchi hiyo kwa manufaa yao binafsi.

Bw. Siala amesisitiza kuwa makundi ya kigaidi yanatumia rasli mali za Libya kuweza kufanikisha ajenda zao ambazo hazina uhusiano wowote na Uislamu.

Na kuongeza kuwa Libya imeridhia mikataba yote ya kitaifa yenye lengo la kupigana dhidi ya ugaidi na inaunga mkono mikakati ya Umoja wa Mataifaya kukabiliana na ugaidi.

Kuhusu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ameomba kufanyike mageuzi ili kuwezesha Afrika iwe na ujumbe wa kudumu katika baraza hilo na kupewa uwezo wa kuwa na kura ya turufu.

 Amesema kuwa hivi sasa Libya inapitisha sheria ili kuweza kujenga upya umoja wa kitaifa na pia kushughulikia changamoto nyingi zinazoikabili nchi hiyo akitolea mfanohaja ya kuwawezesha wanawake na serikali kuheshimu haki za binadamu.

Kuhusu msimamo wa Libya dhidi ya wahamiaji ambao wengi wanatokea Afrika Kusini mwa Jangwa la sahara kutumia taifa hilo kama daraja la kuvuka kwenda kusaka hifadhi na mustakabali bora Ulaya, amesema serikali yake inafanya kila juhudi kuweza kutafuta ufumbuzi dhidi ya  vituo  haramu vinavyowashikilia wahamiaji hao bila kufuata sheria. Lakini akaongeza kuwa  kunahitajika msaada zaidi wa kimataifa kuhusu kukabiliana nasuala hilo.

Pia amepongeza  mkutano ujao wa kuridhia mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji utakaofanyika  mjini Marrakech nchini Morocco Desemba mwaka huu.