Mshikamano ndio suluhu pekee ya maendeleo duniani:Chad

29 Septemba 2018

Ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwa wote duniani , hakuna chaguo lolote la kufikia azma hiyo isipokuwa kufanya kazi pamoja , kuibua vitosho vilivyopo na kukabiliana na changamoto zinazoughubika ulimwengu kwa kuzingatia misingi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi na  waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Chad Mahamat Zene Cherif akihutubia mjadala  wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York, Marekani.

Amewaambia viongozi wa dunia kuwa mkutano wa mwaka huu unazikumbusha nchi zote kuwa hakuna chaguo lolote la kuufikia ubinadamu isipokuwa kushikamana.

Amesema Afrika na hasa eneo la Sahel ikiwemo kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, katikati mwa Mali, Kaskazini mwa Burkanafaso, kusini mwa Algeria , Niger, kaskazini mwa Nigeria, katikati mwa Chad, katikati na kusini mwa Sudan, Kaskazini mwa Sudan kusini, Eritrea, Cameroon, Afrika ya kati na kaskazini mwa Ethiopia, kwa sasa wanakabiliwa na alichokiita vitisho hatari kwani eneo hilo limezungukwa na migogoro na majanga yanavyosababishwa na ugaidi, usafirishaji haramu wa watu, uhalifu wa kimataifa na jangwa.

“Chad imechukua hatua kadhaa kutokomeza hivyo vitisho ambavyo vinaathiri maendeleo. Kuweza kuzishinda changamoto hizi, ushirikiano ni muhimu. Kwa mfano ushirikiano wa nchi za bonde la ziwa Chad zikijumuisha Chad, Cameroon, Niger na Nigeria umesaidia kuwashinda Boko Haram.” Amesema Mahamat.

Amesisitiza kuwa kuhakikisha amani na usalama ni jambo muhimu kwa maendeleo endelevu. Katika kiu yake ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, amani na usalama, mwakilishi huyo wa Chad amesema nchi yake itatoa kipaumbele kwa ushirikiano unaojikita katika matokeo yanayoboresha hali ya maisha kwa watu katika eneo.

Aidha ameongeza kuwa kwa sababu wanawake wana mchango muhimu katika mchakato wa maendeleo, serikali yake ilipitisha sheria mnamo mwezi Mei ya kuhakikisha wanakuwa na asilimia 30 ya wanawake katika utumishi wa umma na nafasi za uongozi wa kuteuliwa.

Kwa nchi za bonde la ziwa Chad amesema majirani hao wanafanya kazi pamoja kuokoa eneo la maji lisipotee lakini hawawezi kufanya hivyo peke yao na hivyo akaomba kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

Akihitimisha hotuba yake amesisitiza umuhimu wa mabadiliko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akijikita zaidi katika haja ya kuwepo kwa kiti au nafasi ya kudumu inayoliwakilisha bara la Afrika katika Baraza hilo.

“Utake usitake” anasema, “Katika karne ya 21, Afrika ni ya muhimu, na sauti yake inatakiwa kusikika”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter