Kwa ujumla usalama umerejea Burundi na wakimbizi wanarudi: Nibigira

Ezéchiel Nibigira, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Burundi akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Ezéchiel Nibigira, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Burundi akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa ujumla usalama umerejea Burundi na wakimbizi wanarudi: Nibigira

Amani na Usalama

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi amesema kwa ujumla hali ya usalama na utulivu imerejea Burundi na kilichosalia ni  matukio madogomadogo ya utovu wa nidhamu.

Akihutubia leo Jumamosi mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 kwa niaba ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo mjini New York Marekani, Bw Ezéchiel Nibigira, amesema hali hiyo shwari ya usalama imewawezesha kuandaa kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi na zoezi kufanyika na kukamilika bila ya tukio lolote baya. Pia hali hiyo imewezesha kufanyika kwa mikutano mbalimbali ya kikanda na kimataifa na kurejea kwa hiyari idadi kuwa ya raia wake walioko ukimbizini nje. Akitaja idadi ya wakimbizi waliorejeanyumbani amesema

“ tangu 2016 wakimbizi zaidi ya 206,000 wamerejea kwa hiari nchini  Burundi. Idadi hiyo inajumulisha wakimbizi 100,000 walioamua kurejea katika mwaka 2016, 168,000 waliorejea Januari hadi Agosti 2017 na pia 38,254 waliorejea baada ya makubaliaono kati ya Burundi, Tanzania na UNHCR.”

Ameongeza kuwa zoezi hilo la kurejea kwa wakimbizi wa Burundi kwa hiari linaednelea. Hata hivyo ameomba Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuyaonya mataifa ambayo yanawazuia raia wa Burundi kurejea kwao kwa hiari. Waziri hakutaja mataifa hayo, lakini ameomba kambi za wakimbizi zisifungwe kwa kuzingatia mkataba wa wakimbizi wa 1951.

Bw. Nibigira akayageukia mataifa ambayo yanawahifadhi wraia wa Burundi walioshiriki katika majaribio ya kuipindua serikali Mei 13 mwaka 2015 kuwarejesha Burundi ili wawajibishwe kisheria kutokana na hatua hiyo.

Na katika siasa ya nchi yake ambayo mara kwa mara zimekuwa zikijadiliwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema mambo yamebadilika na kutaka" Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lazima muwe na ujasiri wa kuiondoa Burundi katika ajenda zenu."

Kuhusu suala la haki za binadamu, waziri huyo, ameumbia mkutano kuwa nchi inarejea kusema kuwa iko tayari kushirikiana na mataifa mengine pamoja na Umoja wa Mataifa kuendeleza  na kulinda haki za binadamu sio Burundi tu lakini hata katika mataifa mengine duniani kwa mujibu wa sheria na mkataba wa haki za binadamu Umoja wa Mataifa.

Masuala mengine aliyogusia katika hotuba yake ni pamoja na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 akitaka viondolewe  akidai kwamba mazingira yaliyopeleka kuviweka yamebadilika kabisa.

Waziri pia ametaka suala la uhamiaji kutatuuliwa  kwa njia bora na kuhusisha mataifa yote wanachama.