Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda itaendelea kuwa kimbilio la wakimbizi- Rugunda

Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda akihutubia Baraza Kuu la UN mkutano wa 73
UN/Cia Pak
Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda akihutubia Baraza Kuu la UN mkutano wa 73

Uganda itaendelea kuwa kimbilio la wakimbizi- Rugunda

Wahamiaji na Wakimbizi

Sisi ni kizazi cha kutokomeza njaaTunaweza kuwa kizazi cha kwanza kufanikiwa kutokomeza njaa, kama ambavyo tunaweza kuwa kizazi cha mwisho kuikoa dunia.

Ni kauli ya Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda akinukuu sehemu ya ujumbe uliomo katika malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs au ajenda 2030 wakati  alipokuwa akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

“Maendeleo yetu na mabadiliko hayawezi hayawezi kupatikana pasipo amani na usalama” anasema Waziri Mkuu Rugunda.

Akizungumzia mzigo wa wakimbizi inaoubeba Uganda, ameutaka ulimwengu kuweka nguvu zaidi katika kuzuia vita na kuhamasisha amani.

“Kama nchi, hivi sasa tunahifadhi wakimbizi milioni 1.4, idadi kubwa zaidi ya wakimbizi barani Afrika na tukiwa katika nafasi za juu kidunia,” amesema.

Hata hivyo Waziri Mkuu Rugunda amesema Uganda itaendelea  kuwa kimbilio la wanaokimbia matatizo katika nchi zao kama litakavyo azimio la New York.

“Tunafanya hivi kwa sababu tunajua kuwa hakuna anayechagua kuwa mkimbizi na tunafahamu umuhimu wa kuwatendea wakimbizi kibinadamu, kistaarabu na kwa heshima”  

Bwana Ruhakana Rugunda amesema ushirikiano kati ya Umoja wa mataifa na Jumuiya za kikanda yamekuwa na faida kubwa katika wajibu wa msingi wa Umoja wa mataifa wa kuhakikisha amani na usalama duniani kote akitolea mfano wa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika AU ulivyosaidia kuboresha amani nchini Somalia.

Amesema tangu vikosi vya muungano wa Afrika vilipoaingia Somalia miaka 11 iliyopita, serikali ya Somalia iliyokuwa ikiendesha nchi ikiwa nje ya Somalia sasa iko Mogadishu tangu mwaka 2007 na kwa hivyo akasema kuwa maendeleo haya chanya na utulivu visingekuwepo kama siyo kwa ushirikiano huo.