Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanahabari 262 wamefungwa mwaka jana pekee, hii si haki:UN

Wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, wakati mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng akiwahutubia.
UN Photo/Ariana Lindquist
Wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, wakati mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng akiwahutubia.

Wanahabari 262 wamefungwa mwaka jana pekee, hii si haki:UN

Haki za binadamu

Waandishi wa mara kwa mara hutishwa, hushambuliwa na hata kuuawa, na idadi kubwa wanafungwa gerezani duniani kote. Hayo yameelezwa bayana na wataalamu wa haki za binadamu kwenye mkutano uliofanyika kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York Marekani.

Wataalam hao wameonya kuwa matukio haya sio tu yanabinya haki za binadamu za wanahabari hao, lakini pia haki ya wanajamii kupokea na kusambaza taarifa.

Mkutano huo umeandaliwa na Kamati ya kuwalinda wanahabari (CPJ), ambalo ni Shirika lisilo la kiserikali la kuhamasisha uhuru wa habari na kupigania haki za waandishi wa habari duniani kote likiwa na makao yake makuu nchini Marekani.

Kwa mujibu CPJ, mwishoni mwa mwaka 2017, wanahabari 262 walifungwa, 70 Uturuki, 40 nchini China na 20 Misri. Takribani asilimia 52 waliofungwa gerezani, ilikuwa ni kwa sababu ya ripoti zao kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ripoti iliyotolewa mwezi Mei mwaka huu wa 2018  na Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO , inasema kufungwa jela kwa wanahabari kusikofuata utaratibu, ambako kunasababisha kupunguza uwazi na uhuru wa wanahabari na pia haki ya watu kupata taarifa, kumeripotiwa kuongezeka ingawa serikali nyingi zinadai kuwa baadhi ya wanahabari wamefungwa kwa sababu ambazo hazihusiani na kazi yao ya uandishi wa habari.

Wapiga picha wakiwa kazini katika chumba maalum cha wanahabari wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjini New York Marekani.
UN Photo/Mark Garten)
Wapiga picha wakiwa kazini katika chumba maalum cha wanahabari wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjini New York Marekani.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa wa CPJ, Joel Simon “Serikali duniani mara nyingi zinatumia sheria za dharura kuvishughulikia vyombo vya habari na wanachokiandika”. Pia wanaleta mashitaka ya madai ya ‘habari za uongo’ dhidi ya waandishi wa habari ambao wanaenda kinyume na matakwa ya Serikali. Wanawashitaki wanahabari katika mahakama za kijeshi na kuwashikilia kwa muda mrefu kabla ya hukumu” 

Ameongeza kuwa “Haya ni matendo ambayo yanaenda kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu, na viwango vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa

Kifungu cha 19 cha Azimio la Haki za Binadamu kinasisitiza“Uhuru wa kuwa na maoni bila kuingiliwa na haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa na mawazo kupitia vyombo vyovyote na bila kujali mipaka”. Mwaka 2013, Baraza Kuuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha tarehe mbili ya mwezi Novemba kuwa siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili na uhalifu dhidi ya wanahabari, vitendo ambayo vinaendelea kuonekana duniani kote.

Mkutano huu uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa umezungumzia pia kesi tano mahususi za wanahabari ambao wamefungwa kwa sasa akiwamo: Alaa Abdelfattah kutoka Misri na Azimjon Askarov kutoka Kyrgyzstan, hawa walikaamatwa wakifuatilia kinachosemekana kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama; Shahidul Alam kutoka Bangladesh alifungwa alipokuwa akiripoti mgomo wa wanafunzi; na kesi nyingine kubwa ni ile ya wanahabari wawili wa Reuters nchini Mynmar, Kyaw Soe Oo kwa jina lingine Moe Aung na Wa Lone pia akifahamika kwa jina Thet Oo Maung waliohukumiwa miaka 7 gerezani kwa mashitaka ya kuvunja sheria ya kutoboa siri za nchi walipokuwa wakiripoti taarifa za mauaji ya warohingya yaliyotekelezwa na majeshi ya Mynmar mwezi septemba mwaka 2017.

Wanahabari na wahudhuriaji wengine wa tukio la kupiga kengele ya amani katika siku ya amani duniani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Wanahabari na wahudhuriaji wengine wa tukio la kupiga kengele ya amani katika siku ya amani duniani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mapema mwezi huu wa septemba, kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet alisema kazi waliyokuwa wanaifanya wanahabari kuripoti tukio hilo la mauaji nchini Mynmar ambako majeshi yamekiri kuhusika, ilikuwa ni kazi ambayo ni muhimu kwa jamii vinginevyo bila wanahabari hao tukio hilo lisingefahamika na hivyo akatoa wito hukumu yao itenguliwe na waachiwe pamoja na wanahabari wengine walioko kizuizini kutokana na kutimiza haki na uhuru wao wa kujieleza.