Chonde chonde Umoja wa Mataifa tuondoleeni vikwazo vya silaha:Somalia

29 Septemba 2018

Ninausihi Umoja wa Mataifa kuiondolea Somalia vikwazo vya ununuzi wa silaha . Wito huo umetolewa leo na Ahmed Isse Awad Waziri wa mambo ya nje wa Somalia akihutubia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 mjini New York Marekani hii leo.

Waziri huyo amewaambia viongozi wenzake kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa zuio hilo kwa Somalia la kutonunua silaha limekuwepo kwa muda mrefu na ndilo hasa linakwamisha mapambano yao dhidi ya makundi ya kigaidi. 
 
“Vikosi vyetu vinapokuwa na silaha za mapambano kama zile walizonazo maadui zetu, uwezekano wa ushindi unakuwa nusu kwa nusu. Uwezo mkubwa wa kupigana utatuwezesha kuwa na nafasi ya juu na kuwaangamiza kabisa magaidi na pengine katika muda mfupi” 

amesema  Waziri Ahmed ambaye amemuwakilisha Rais Mohamed Abdullah Mohamed anayeiongoza Somalia kwa mwaka mmoja na nusu sasa.
 
Ameongeza kuwa Somalia imeanzisha duru ya pili ya operesheni ambazo zimefanikiwa kufungua mtandao wa barabara na wameweza kukomboa miji na vijiji kadhaa kutoka katika mikono ya magaidi wa Al-Shabaab.
 
Ameeleza kuwa wao pamoja na washirika wao wamefanikiwa kuyaharibu maficho ya magaidi, huku wanawahusisha viongozi wa kidini, wazee, vijana, wanawake na makundi ya kijamii kubadilisha mtazamo wa chuki na hali ya kutovumiliana katika imani za dini.
 
Waziri huyo amesisitiza  “Na kizuri ni kwamba vijana wadogo na wanawake hawajiungi na Alshabab kwa kutaka. Hilo siyo maarufu tena; Alshabab na Alqaed hawana watu wapya na wale wa kujitolea nchini Somalia” 
 
Pia amesema kupitia msamaha walioutoa, vijana wengi na wanawake wameachana na vurugu na wamejisalimisha kwa amani.
 
“Makamanda wa ngazi ya juu, viongozi na wapiganaji pia, bila masharti wamejisalimisha wakija na silaha pamoja na magari ya kijeshi ambayo katika maneno ya kijeshi yanaitwa “Technicals”.
 
Hatua ambayo amesema imedhoofisha zaidi mtandao wa kigaidi na uwezo wao wa kupanga na pia akasema, “ Kiu yetu ya amani na Somalia iliyotulia haitaishia kwa kuwashinda Alshabab, lakini hii ni hatua ya kwanza”.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter