MachafukoYemen yasababisha misaada kusitishwa: OCHA
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA nchini Yemen, Jamie McGoldrick ameomba kusitishwa kwa utoaji wa huduma za kibinadamu nchini humo baada ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengi katika mji mkuu Sanaa.
Bwana McGoldrick amesema hali ya usalama kwa watoa huduma wa mashirika tofauti ni hatarishi kutokana na migogoro ya hivi karibuni.
Amesema mitaa ya mji wa Sanaa ni sawa na uwanja wa vita , wananchi wamekwama majumbani , hivyo uwezo wa kuwafikishia misaada na huduma ni mdogo na hatarishi.
Aidha amesema watoa huduma wanazidi kupokea simu za uhitaji kutoka kwa maelfu ya wananchi wenye uhitaji wa vitu mbalimbali ikiwemo dawa, chakula, maji, mafuta ya taa, ila watoa huduma wanashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia usalama wao.
Mkuu huyo wa OCHA nchini Yemen anatoa wito kwa pande zote kinzani na pia nchi wanachama wenye nafasi ya kusaidia kusitisha mapigano, ili mashirika ya kibinadamu yaweze kuwafikia wananchi walio katika hali ya uhitaji mkubwa ambao asilimia kubwa ni wanawake watoto na wazee wasiojiweza.