Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaomba usaidizi kwa wadau kukabiliana na kipindupindu katika nchi 11 Afrika

Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.
© UNICEF
Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.

UNICEF yaomba usaidizi kwa wadau kukabiliana na kipindupindu katika nchi 11 Afrika

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuhudumia watoto UNICEF limetoa ombi la dola milioni 171 ili liweze kusaidia watu milioni 28 wanaokabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu katika nchi 11 zilizokopo Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika.

Nchi hizo 11 ambazo ni Malawi, Msumbiji, Somalia, Kenya, Ethiopia, Zambia, Sudan Kusini, Burundi, Tanzania, Zimbabwe na Afrika Kusini kwa sasa zinapambana na milipuko mbaya zaidi ya kipindupindu kuwahi kukumba eneo hilo kwa miaka mingi.

Taarifa iliyochapishwa leo kwenye wavuti wa UNICEF imesema wanalenga kuhamasisha usaidizi muhimu wa kuokoa maisha, unaojumuisha vifaa vya dharura vya afya, bidhaa za matibabu, msaada wa kiufundi kwa udhibiti wa milipuko, mawasiliano ya hatari na ushiriki wa jamii kwa ajili ya kuzuia kusambaa zaidi na matibabu ya mapema, pamoja na maji safi, salama na lishe.

Shirika hilo pia limesema linashughulikia ulinzi wa kijamii na kusaidia maisha, pamoja na kuwaweka watoto salama na kujifunza.

Misaada inatofautiana kwa kila nchi

Pamoja na kuwa fedha zinahitaji kwa ajili ya nchi 11 UNICEF imesema imeandaa mipango binafsi kwa kila nchi ili kuweza kukabiliana na kipindupindu kulingana na hali ya kipekee ya ndani ya nchi iliyoathiriwa.

Madhalani nchini Msumbiji na Malawi, bajeti zao zinajibu mahitaji ya athari zilizoletwa na mafuriko yalitozikumba nchi hizo hivi karibuni ambayo yamechangia kuenea kwa kipindupindu.

Tayari mpaka sasa wadau wa UNICEF wamechangia dola milioni 18.3 kwa ajili ya waathirika wa kipindupindu Mashariki na Kusini mwa Afrika, na fedha hizo zimesaidia kwenye usafishaji wa maji, udhibiti wa maambukizi na kampeni za kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo na namna ya kujikinga na kupata huduma za mapema.

Hata hivyo bado kuna upungufu wa ziaid ya 89% hali inafanya UNICEF kushindwa kukidhi mahitaji kamili ya watoto na wanawake walioathiwa na kipindupindu.