Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto katika nchi 11 za Mashariki na Kusini mwa Afrika wako hatarini sababu ya kipindupindu: UNICEF

Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.
© UNICEF
Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.

Watoto katika nchi 11 za Mashariki na Kusini mwa Afrika wako hatarini sababu ya kipindupindu: UNICEF

Afya

Nchi 11 Mashariki na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na hali mbaya ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambako hadi sasa kumeripotiwa wagonjwa 67,822 na vifo 1, 788 kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Nairobi, Johannesburg na New york inasema huenda idadi kamili ya wagonjwa na vifo ikawa kubwa zaidi kutokana na changamoto ya mifumo ya ufuatiliaji, utoaji taarifa na unyanyapaa.

Nchi mbili ambazo zina mzigo mkubwa zaidi ni Malawi na Msumbuji ambazo shirika hilo linasema kwa pamoja zaidi ya watu milioni 5.4 wanahitaji msaada wakiwemo watoto zaidi ya milioni 2.8.”

Naibu mkurugenzi wa kinanda wa UNICEF Lieke van de Wiel ambaye amehudhuria mkutano wa mawaziri kuhusu kipindupindu mjini Lilongwe Malawi amesema “Tulifikiri ukanda huu hautoshuhudia mlipuko wa kipindupindu wa kiwango hiki cha kusambaa kwa zama hizi. Mifumo duni yam aji na usafi, matukio mabaya ya hali ya hewa, mizozo inayoendelea na mifumo duni ya afya vimezidisha adha na kuweka rehani maisha ya mamilioni ya watoto kote Kusini mwa Afrika.”

Msaada wa UNICEF katika ngazi za kitaifa unajumuisha “utoaji wa maji safi na huduma ya usafi, kuweka tembe za kusafisha maji, sabuni za kunawia mikono,dawa za kuongeza maji mwilini, huduma ya kubadili mwenendo wa tabia, na kusambaza ujumbe wa kampeni ya kuishirikisha jamii na zaidi ya hayo UNICEf na washirika wake pia wanatoa msaada wa vifaa vya afya na mahema kwa ajili ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha wagonjwa.”

Kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali hususani katika nchi zilizoathirika zaidi na kipindupindu sasa “UNICEF inaomba dola milioni 150 kwa aajili ya kuzisaidia nchi zote 11 zilizoathirika ikiwemo dola milioni 34.9 kwa ajili ya Malawi, na milioni dola 21.6 kwa ajili ya Msumbiji kuweza kutoa huduma za kuokoa Maisha kwa watu walioathirika na mlipuko huo.”

Hadi sasa washirika wa UNICEF wameshachangia dola milioni 2.9 kukabiliana na mlipuko nchini Malawili na dola 550,000 kwa ajili ya Msumbiji.