UNGA77 yafunga pazia, Afrika yasema sasa ni wakati wa kuwa na ujumbe wa kudumu

Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 umekunja jamvi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa ukiwa na maudhui: Wakati muhimu: Majawabu ya kuleta marekebisho kwa changamoto zinazofungamana. Katika siku 6 za mjadala huo nchi za Afrika zilitumia fursa kuhoji marekebisho gani yanawezekana bila kurekebisha chombo hicho ambacho kura yenye maamuzi ya msingi inamilikiwa na wanachama 5 kati ya 193, ikiwa ni miaka 77 tangu kuudwa kwake.
Baraza la Usalama la UN ambalo lina jukumu la amani na usalama duniani lina wajumbe 15 kati yao 5 ambao ni Urusi, Uingereza, Marekani, China na Ufaransa ni wa kudumu na wana kura turufu au veto ambayo ikipigwa na mmoja wao basi hoja iliyoko mezani inapita au inakataliwa hata kama wengine 14 wamekubali.
Baadhi ya viongozi wa Afrika wanahoji “Je kwa hali hii kutakuwa na mabadiliko yoyote wakati huu Baraza la Usalama linapaswa kuamua mambo makuu yanayotishia usalama duniani kuanzia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, vikundi vilivyojihami jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC, ghasia Sudan Kusini na kwingineko? Viongozi wa Afrika wamesema nini?”
Ni kwa mantiki hiyo wakafunguka mathalani Demeke Mekonnen, Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia akishikilia pia wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje akihutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akisema, Afrika haina ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama! Azma yetu ya majawabu ya kiafrika kwa changamoto za Afrika bado haijapatiwa heshima na msaada unaohitajika!
Amesema “changamoto za Afrika zitashughulikiwa kwa uendelevu pale tutakapozifuatilia kwa kuzingatia hali halisi ya ukanda huo na kuzingatia maslahi ya kimkakati na matarajio ya nchi husika! Ni pale tu tutakapozingatia majawabu ya kikanda ndipo tutaanza kupunguza hoja za Afrika zisizoisha kwenye Baraza la Usalama.”
Afrika Kusini ambayo Waziri wake wa Uhusiano wa kimataifa na Ushirikiano Dkt. Grace Naledi Pandor akahoji ni kwa vipi Umoja wa Mataifa unaweza kupata majawabu ya kuleta marekebisho bila kwanza kujirekebisha yenyewe, akisema “haikubaliki miaka 77 tangu kuanzishwa kwake, mataifa matano ndio yanamiliki nguvu ya maamuzi kwenye mfumo wote wa Umoja wa Mataifa. Ili Umoja wa Mataifa uwe fanisi, Baraza Kuu lazima liimarishwe na Baraza la Usalama lirekebishwe.”
Kwa Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, yeye alirejelea makubaliano ya Ezulwini ya mwaka 2005 baina ya nchi za Afrika kuhusu marekebisho ya mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais Chakwera anasema, “sisi nchi wanachama kutoka Afrika, hatutamani kukutana tena hapa mwakani bila maendeleo yoyote kuhusu makubaliano ya Muungano wa Afrika ya Ezulwini yanayotaka viti viwili vya kudumu vyenye kura turufu na viti vitano visivyo vya kudumu kwa Afrika.”
Amesema matarajio yao ni kuona suala hilo likielekea Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwasilishwa mezani, lisikilizwe na litatuliwe. Huu ndio Umoja wa Mataifa tuutakao. Ndio Umoja wa Mataifa dunia inahitaji. Umoja wa Mataifa unaotekeleza Demokrasia inayohubiri.
Jamhuri ya Afrika ya Kati iliwakilishwa na Rais wake Faustine- Archange Touadera ambaye alisema iwapo jukumu la Umoja wa Mataifa ni kurekebisha dunia, kuifanya kuwa pahala pa haki zaidi basi ni lazima ujirekebishe.
Amesema Jamhuri ya Afrika ya Kati inasisitiza kuunga kwake mkono msimamo wetu wa Muungano wa Afrika, ambao unataka marekebisho ya kina ya Umoja wa Mataifa na kupanua idadi ya wajumbe kwenye Baraza la Usalama kwa uwakilishi sawa na uwakilishi zaidi wa mabara yote.
Kwa upande wake, Jamhuri ya Congo, hoja ya Afrika kuwa na ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama imefananishwa na nyoka atelezaye baharini, hakamatiki na anayoyoma kila anapotaka kukamatwa. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Jean-Claude Gakosso amesema, “Afrika lazima ichukue nafasi yake katika jamii ya kimataifa, na kufikiria vinginevyo ni kuonesha ubinafsi na kwenda kinyume na mwelekeo wa historia,”
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria akamulika changamoto lukuki zinazokabili dunia kuanzia amani na usalama, haki za binadamu, maendeleo na mabadiliko ya tabianchi akisema, « Bado nasalia kushawishika kuwa changamoto zinazoibuka kwa wingi katika miezi na miaka ya hivi karibuni zinasisitiza wito wa Nigeria na nchi nyingine nyingi za Afrika za marekebisho ya Baraza la Usalama na mashirika mengine ya Umoja wa MAtaifa. »
Kutoka Afrika Mashariki hususan nchini Tanzania Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akihutubia UNGA77 akaunga mkono makubaliano ya Ezulwini na azimio la Sirte kuhusu ujumbe wa kudumu wa Afrika kwenye Baraza la Usalama akisema,
“ Uhalali wa Umoja wa Mataifa unategemea Baraza la Usalama lenye uwakilishi sawia na linalochukua hatua.Tumechelewa sana kwa Umoja wa Mataifa kuakisi uhalisia wa zama za sasa na si zama za miaka ya 1940.”
Kwa Uganda hoja ya marekebisho ya Baraza la Usalama ni suala la dharura hivi sasa kuliko wakati wowote, amesema Makamu wa Rais wa Uganda Bi. Jessica Alupo akisema, “Afrika ikiwa na zaidi ya wakazi bilioni moja na zaidi ya asilimia 70 ya ajenda za Baraza la usalama ni za Afrika, bado inaendelea kuumizwa na ukosefu wa haki wa kihistoria kwa kutokuwa na ujumbe wa kudumu kwenye Baraza halikadhalika idadi ndogo kwenye ujumbe usio wa kudumu.”
Hoja hiyo ya nchi za Afrika ilipatiwa msukumo zaidi na Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza kuu la Umoja wa MAtaifa Csaba Kőrösi ambaye katika hotuba yake amesisitiza kuendelea kuimarishwa sio tu kwa Umoja wa Mataifa balipia Baraza Kuu akisema uwezo wa kuimarisha vyombo hivyo utadhihirisha uhalali wake kwa macho ya wakazi wa dunia na zaidi ya yote ni Baraza la Usalama akisema, “nataka kusongesha mashauriano kuhusu marekebisho ya Baraza la Usalama: Ni wakati sasa kwa Baraza kuwakilisha idadi ya wakazi wa dunia kwa usawa zaidi, na kwamba liakisi uhalisia wa karne ya 21. Hili ni suala la uhalali wa shirika letu lote na hali ya ushirikiano wa kimataifa.”