Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA ‘kupitisha kikombe’ kusongesha operesheni zake

Mwanamke anapokea msaada kutoka UNRWA. Picha: UNRWA

UNRWA ‘kupitisha kikombe’ kusongesha operesheni zake

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wapalestina, UNRWA limeanzisha kampeni ya kuchangisha fedha ili kuweza kutekeleza operesheni zake, ikiwa ni mara ya kwanza kuchukua hatua hiyo tangu lianze operesheni zake mwaka 1950. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Hiyo ni moja ya hatua ambazo imechukua kufuatia kitendo cha Marekani kupunguza mchango wake kutoka dola milioni 350 hadi dola milioni 60.

Kamishna Mkuu wa UNRWA Pierre Krähenbühl kupitia taarifa yake ametaja hatua nyingine kuwa ni wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kusimama kidete na kuungana na UNRWA kupazia haki na mustakhbali wa wakimbizi wa Palestina.

Halikadhalka ametoa wito kwa wadau, nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Palestina pamoja na wahisani kusaidia kuanzisha vyanzo vipya vya fedha ili kuhakikisha wakimbizi wa Palestina wanaendelea kupata elimu na kwamba utu wa watoto na familia za kipalestina unalindwa.

Mapema akizungumzia hatua ya Marekani kukata mgao wake kwa UNRWA, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema..

(Sauti yaAntonio Guterres)

“Kwa hiyo iwapo UNRWA haitakuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu na zile za dharura ambapo imekuwa ikitoa, hii itasabaisha tatizo kubwa. Na tutafanya kila tuwezalo kuepusha hali hii isitokee.”