Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usaidizi wetu DRC uko njiapanda- IOM

Wakimbizi wa ndani DRC. Picha: IOM

Usaidizi wetu DRC uko njiapanda- IOM

Hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC iko njia panda kama ulivyo uwezo wa kifedha wa kuweza kushughulikia hali hiyo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM hii leo . Siraj Kalyango na taarifa kamili.

(Taarifa ya Siraj Kalyango)

IOM imesema hali ya kibinadamu DRC inazorota kila uchao kadri mapigano yanavyozidi kushamiri hususan kwenye majimbo ya Tanganyika na Kasai.

Mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu pamoja na mafuriko ya hivi karibuni vimezidi kuongeza marudufu mahitaji ya kibinadamu pamoja na yale ya kiafya.

Mazingira hayo yamesababisha ongezeko la idadi ya wakimbizi wa ndani huko Kasai na jimbo la Kivu Kaskazini na Tanganyika, ambapo simulizi za wananchi juu ya madhila waliyokumbana  kama vile kubakwa, mateso na mauaji ya wapendwa wao zikitia huzuni kubwa.

Mkuu wa IOM huko DRC Jean-Philippe Chauzy akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi amesema ingawa mahitaji yanaongezeka bado ombi la fedha la mwaka jana kwa ajili ya kutekeleza opereshani zake bado halijatimizwa. Hivyo amesema…

(Sauti ya Jean-Philippe Chauzy)

“Ombi la mwaka jana la lilifadhiliwa kwa chini ya asilimia 50 au lilizidi kwa asilimia 51 mwishoni mwa mwka 2017, lakini bado limechangiwa kidogo sana. Na mwaka huu tunatangaza ombi la dola bilioni Moja nukta Sita Nane, tunatarajia kupata fedha hizi kwa sababu mahitaji yapo na hatuwezi kuacha hivi hivi DRC.”