Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wengine 100 wahofiwa kufa maji Mediteranea

Watu wanaovuka bahari ya mediterranea kutoka Afrika kasakzini.(Picha:UNHCR)

Wahamiaji wengine 100 wahofiwa kufa maji Mediteranea

Mwaka wa 2018 umeanza vibaya kwa wasaka hifadhi ambapo yaelezwa wahamiaji wapatao 100 wahofiwa kuzama maji kwenye bahari ya Mediteranea. Selina Jerobon na ripoti kamili.

(Taarifa ya Selina Jerobon)

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limenukuu walinzi wa pwani ya Libya wakisema kuwa wahamiaji hao walikuwemo kwenye boti ya tatu ambayo nayo iliripotiwa kuzama jana,

Christine Petré kutoka IOM amesema boti zilizokuwa zimebeba wahamiaji hao ziliondoka miji ya pwani ya Azzawiyah na Al Khums nchini Libya zikiwa zimechukua wahamiaji wengi kutoka nchi za Gambia, Senegal, Sudan, Mali, na Nigeria.

Wahamiaji hao wanaokwenda Ulaya wameripotiwa kupoteza maisha kwenye eneo la bahari ya Mediteranea kati ya Hispania na Morocco na wengine ni kati ya Italia na Libya.

IOM inasema tukio hili linafanya idadi ya watu wanaohofiwa kufa maji Mediteranea kufikia takribani 200 tangu kuanza kwa mwaka huu ikijumuisha na waliokuwemo kwenye boti nyingine mbili, wakiwemo wanawake na watoto.

Idadi hii kwa mujibu wa IOM ni kikubwa wakati ambapo mwezi uliopita pekee idadi ya vifo ilipungua kwa kiasi kikubwa, hivyo idadi ya sasa inaonyesha kuwa pengine mwaka 2018 unaweza kuwa mbaya zaidi kwa wasaka hifadhi Ulaya.

IOM nchini Libya inaendelea kuwapatia usaidizi manusura wa zahma hiyo ya hivi karibuni huku ikitaka hatua zaidi zichukuliwe ili kudhibiti safari hizi zisizo salama.