Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japan yasaidia kuimarisha ulinzi wa amani

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wapiga doria. Picha: MINUSMA/Sylvain Liechti

Japan yasaidia kuimarisha ulinzi wa amani

Mkuu wa operesheni za amani mashinani kwenye Umoja wa Mataifa Atul Khare  amesema mradi wa pande tatu unaohusisha Japan, Afrika na Umoja wa Mataifa umezaa matunda katika kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Bwana Khare amesema mradi huo unafadhiliwa na Japan na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa huku nchi za afrika zikitoa wanajeshi wanaofanyiwa mafunzo ya uhandisi wa kutengeneza vifaa vinavyotumika vitani wakati wa kulinda amani.

(Sauti ya Atul Khare)

“Na watu wengi ambao wamepata mafunzo hayo wamekwisha pelekwa katika sehemu za kulinda amani, na idadi kubwa wamepelekwa AMISOM,  ambapo kama mnavyojua ndio sehemu kubwa ambayo Umoja wa Mataifa umepeleka walinda amani wake.”

Amesema tayari Brazil imeonesha nia ya kujiunga kwenye programu hiyo na wanakaribisha wadau wakati huu wakiangalia namna ya kuipeleka katika mabara mengine kama Asia na  Amerika ya kusini

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani mashinani amesema mwaka 2017 umekuwa ni mbaya kwa ulinzi wa amani kwani ni watu 123 wamefariki dunia, ambapo 60 kati yao  ni walinda amani na wengine watumishi wa kawaida.

Ameongeza kuwa tayari wameshaanza kuchunguza shambulio la hivi karibuni lililosababisha walinda amani 15 kutoka nchini Tanzania kufariki dunia.

Idadi hiyo ya vifo imeongezeka baada ya mlinda amani mwingine aliyekuwa anatibiwa huko hospitali ya Mulago nchini Uganda kufariki dunia hii leo.