Ukatili na mauaji vyaendelea Sudani Kusini- Ripoti

Ripoti ya watalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa wiki hii imesema baada ya miaka minne ya machafuko nchini Sudan Kusini imebanika kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na pande kinzani uliosababisha maisha ya watu wengi wasio na hatia kupotea.
Wataalamu hao walifanya uchunguzi kwa ushirikiano na IGAD, nchini Sudan Kusini, Mashariki mwa Ethiopia na kaskazini mwa Uganda kuanzia tarehe 11 had 22 Disemba na kuwasilisha ripoti hiyo huko Addis Ababa.
Ripoti imebaini kuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo vitendo vya utekwaji nyara kwa watoto, ubakaji kwa wanawake na wasichana, mauaji, uporaji wa mali za wananchi, uchomwaji wa makazi ya watu na pia ukimibizi wa ndani kwa mamilioni ya raia.
Profesa Andrew Claphan wa ofisi ya haki za binadamu amesema walishtushwa na ushahidi kutoka kwa waathirika wakati wakitembelea Sudan Kusini katika jitihada za kukusanya taarifa kwa waathirika wa ukatili hususan wanawake walipokuwa wanaeleza kuhusu vitendo vya ubakaji walivyofanyiwa.
Ofisi ya haki za binadamu imetoa wito kwa pande zote kinzani kusitisha mapigano mara moja na kukaa kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro huu ili kuokoa maisha ya mamilioni ya raia wasiokuwa na hatia na pia kuruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie walengwa..