Chanjo milioni 1.4 za homa ya manjano kuokoa maisha Nigeria:WHO

1 Disemba 2017

Kundi la kimataifa la kuratibu utoaji wa chanjo ya homa ya manjano (ICG) limetoa dozi  milioni 1.4 za chanjo ya homa ya manjano kwa ajili ya kampeni itakayoanza kesho Jumamosi Desemba pili ili kusaidia kudhibiti mlipuko wa homa ya manajano unaoendelea nchini Nigeria.

Serikali ya Nigeria kwa msaada wa shirika la afya ulimwenguni WHO na wadau wengine inatarajiwa kuwachanja watu milioni 1.3 katika kudhibiti mlipuko huo kwenye maeneo yaliyoathirika.

Chanjo hiyo inayofadhiliwa na muungano wa chanjo duniani Gavi itatolewa katika baadhi ya sehemu za jimbo la Zamfara  ambako visa vya homa ya manjano vimethibitishwa.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa WHO nchini Nigeria Dr Wondimagegnehu Alemu, shirika hilo linashirikiana na serikali ya Nigeria ili kushughulikia kinga dhoofu miongoni mwa jamii ambayo inasababisha kuongezeka kwa visa vya homa ya manjano.

Kutolewa kwa dozi milioni 1.4 za chanjo hizo kunafuatia juhudi zizlizoanza Oktoba ambapo watu 874,000 walifikiwa na chanjo katika majimbo ya Kwara na Kogi. Hadi kufikia Novemba 21 visa 276 vya homa ya manjano vimeripotiwa katika majimbo 21 ya Nigeria.

Duru hii ya kampeni itawalinda watu Zaidi ya milioni moja Nigeria, itaokoa maisha na inatarajiwa kuepusha mlipuko utakaosababisha madhara makubwa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter