Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya chanjo kwa watoto wa Rohingya yaanza :UNICEF/WHO

Msichana mdogo anabeba mtoto mgonjwa kwenye Kituo cha Matibabu cha Jeshi katika Kambi ya Wakimbizi ya Kutupalong, Makazi ya muda. Picha: OCHA / Anthony Burke

Kampeni ya chanjo kwa watoto wa Rohingya yaanza :UNICEF/WHO

Serikali ya Bangladeshi kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la afya duniani WHO na muungano wa chanjo GAVI, leo wamezindua kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa dondakoo na magonjwa mengine yanayozuilika kwa watoto wote wakimbizi wa Rohngya walio na umri wa kati ya wiki sita hadi miaka 6.

Watoto hao ni wanaoishi katika makambi 12 na makazi ya muda karibu na mpaka wa Myanimar. Kwa mujibu wa mashirika hayo chanjo hii ya haraka itawahusisha watoto takribani 255,000 katika wilya za Ukhiya na Teknaf kwenye viunga vya Cox’s Bazar, wakati serikali na wadau wengine wa afya wakiendelea kuongeza msaada wa matibabu ya dondakoo na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Mwakilishi wa UNICEF Bangladesh Edouard Beigbeder, amesema mlipuko wa dondakoo unaonekana kuongezeka hali inayowaweka watoto hao wakimbizi katika hatari kubwa huku takwimu za WHO zikionyesha kwamba kuna visa 722 vinavyoshukiwa na vifo 9 miongoni mwa watoto.

Chanzo zingine watakazopewa watoto hao kwa awamu ni za, pepopunda, mafua, Homa ya aini aina B, polio na kifaduro.