Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Serge Brammertz Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya UM juu ya Makosa ya Vita kwa iliokuwa Yugoslavia (ICTR) amewasilisha ripoti maalumu kwa waandishi habari Ijumatatu (21 Julai) ya kupongeza kukamatwa kwa Radovan Karadzic, kiongozi wa kisiasa wa Waserb wa Bosnia na mtoro aliyekimbia adhabu ya sheria kwa muda mrefu katika Bosnia-Herzegovina. Karadzic alishikwa na wenye madaraka Serbia na sasa yupo kizuizini. Karadzic alishitakiwa rasmi na Mahakama ya ICTR miaka 13 iliopita kwa kuongoza makosa dhidi ya utu na mauaji ya halaiki kwa raia wa Bosnia-Herzegovina wasiokuwa Waserb - yaani Wacroat na WaIslamu wa huko. Tutakupatieni taarifa zaidi Ijumanne.

Msanii wa Sudan Kusini ataka biashara ya silaha ndogo ndogo ikomeshwe

Wiki hii kwenye Makao Makuu ya UM kulifanyika mkutano wa kutathminia hatua za kukomesha matatizo yanayoambatana na biashara haramu ya silaha ndogo ndogo. Mkutano huu hujumuisha Mataifa Wanachama kila miaka miwili ambapo huwapatia wajumbe wanaohudhuria kikao fursa ya kubadilishana mawazo juu ya uzoefu walionao, na kujadilia namna ya kukwamua vile vizingiti vyenye kutatanisha utekelezaji wa Mpango wa Utendaji wa 2001 (PoA) dhidi ya biashara haramu ya silaha ndogo ndogo duniani, silaha ambazo pia hutumiwa kupalilia vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi masikini.~

Ripoti ya IMF kuhusu uchumi wa dunia ina matokeo ya mchanganyiko

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limewasilisha ripoti maalumu inayokadiria Matarajio ya Uchumi Duniani kwa 2008-2009. Ripoti hii hutolewa kila baada ya miezi mitatu na ina mwelekeo wa kutia moyo. Ripoti ilisisitiza kwamba ijapokuwa uchumi wa dunia umeopnekana kuzorota mwaka huu na unakuwa kwa kiwango cha chini, kwa asilimia nne tu, wataalamu bado wanaamini na kubashiria tutashuhudia muongezeko wa kuridhisha mwaka huu na katika kipindi kitakachoanzia nusu ya pili ya 2009, kwa kiwango cha wastani.

Djibouti inakurubia ukingo wa janga la njaa, WFP yaonya

Dally Belgasami, Mkurugenzi wa Ofisi ya Geneva ya Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) aliwaarifu waandishi habari kwamba Djibouti ipo ukingoni mwa janga la njaa ya halaiki na inahitajia kufadhiliwa, kidharura, msaada wa chakula na wahisani wa kimataifa ili kunusuru umma na vifo.

UNHCR imepungukiwa fedha za kuhudumia wahamiaji wa Sudan Kusini

Jennifer Pagonis, Msemaji wa Geneva wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ameripoti kwa waandishi habari kuwa taasisi yao inakabiliwa na upungufu wa dola, karibu milioni 12, zinazotakiwa kushughulikia operesheni za kuwasaidia kihali wahamiaji wa Sudan Kusini waliodhamiria kurudi mwakao katika nusu ya pili ya mwaka. Huduma hizi zikikamilishwa zitawapatia wahamiaji hawo uwezo wa kuanzisha maisha mapya.

Sera ya EU kudhibiti wahamiaji yashtusha wataalamu wa haki za binadamu wa UM

Wataalamu kumi wanaohusika na Masuala Makhsusi ya Baraza la Haki za Binadamu wamemtumia barua maalumu Raisi wa Baraza la Umoja wa Ulaya, uraisi ambao unashikwa na Ufaransa kwa sasa, inayobainisha wasiwasi wao kuhusu pendekezo la \'Mwongozo wa EU juu ya Udhibiti wa Uhamiaji\' kwenye nchi wanachama wa EU. Sera imependekeza mataifa yote yakubali kutekeleza kipamoja sheria za kuwarejesha makwao, bila khiyari, wale raia wwenye kuishi kwenye mataifa ya EU ambao waliokiuka ruhusa ya muda wa ukaazi.

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limekutana Ijumaa kuzingatai shughuli za Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) na pia kufanya mapitio ya ripoti ya KM kuhusu ombi la Nepal la kutaka UM usaidie kuimarisha mpango wa amani nchini humo. Baraza la Usalama limeamua kuongeza muda wa kazi kwa majaji wanaohusika na mauaji ya Rwanda, ili kuhakikisha kesi zilizosalia zinakamilishwa kwa muda unaotakiwa na ICTR.

Watumishi wa WHO wanajiandaa kurejea Iraq

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza wafanyakazi wa kimataifa walioondoshwa Iraq baada ya shambulio la Ofisi za UM za Baghdad katika Agosti 2003, wanajiandaa sasa hivi kurudi tena nchini humo kutekeleza majukumu yao. WHO imesisitiza hatua hii itaisaidia Iraq kukabiliana vizuri zaidi na matatizo ya kiutu yaliojiri nchini, na vile vile itaipatia marekibisho yanayohitajika kuimarisha vizuri zaidi sekta ya afya ya jamii, hasa kwenye mazingira magumu ambayo yametanda Iraq kwa sasa. ~~