Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya IMF kuhusu uchumi wa dunia ina matokeo ya mchanganyiko

Ripoti ya IMF kuhusu uchumi wa dunia ina matokeo ya mchanganyiko

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limewasilisha ripoti maalumu inayokadiria Matarajio ya Uchumi Duniani kwa 2008-2009. Ripoti hii hutolewa kila baada ya miezi mitatu na ina mwelekeo wa kutia moyo. Ripoti ilisisitiza kwamba ijapokuwa uchumi wa dunia umeopnekana kuzorota mwaka huu na unakuwa kwa kiwango cha chini, kwa asilimia nne tu, wataalamu bado wanaamini na kubashiria tutashuhudia muongezeko wa kuridhisha mwaka huu na katika kipindi kitakachoanzia nusu ya pili ya 2009, kwa kiwango cha wastani.

Lakini ripoti ilisema mifumo ya fedha, hasa katika nchi zenye maendeleo ya viwanda, imeghumiwa na hali ya kigeugeu, na inahitajia marekibisho ya haraka, hasa kwenye zile sekta za mabenki yenye kutoa mikopo kinga ya kununua nyumba. Kwa sababu katika miezi ya karibuni, harakati za kuendesha shughuli hizi ziliporomoka na athari zake zilipamba sekta kadha nyenginezo za uchumi na jamii na kutifua mregezo wa matumizi fedha za kuendesha shughuli za benki kwa sababu ya kudidimia kwa akiba. IMF inakhofia hali hii kama haijadhibitiwa mapema huenda ikavuruga utabiri wao kwenye siku zijazo. Lakini Mshauri Johnson wa IMF, alidhihirisha kwenye taarifa yake kuwa na imani kubwa juu kurejea kwa utulivu wa kuridhisha shughuli za biashara kwenye soko la fedha, kwa sababu taasisi kadha zinazoendesha mabenki zilishafadhiliwa mitaji ziada kukabiliana na mgogoro wa fedha na serikali zao.

Kadhalika, ripoti ya IMF ilitahadahrisha ya kuwa mifumko ya bei za vitu na bidhaa ulimwenguni ni tatizo linalohitajia kuchungwa sana, na kupatiwa suluhu ya haraka, ya muda mrefu, au si hivyo soko la kimataifa halitomudu kurudisha utulivu unotakikana kuongoza shughuli za kiuchumi zenye natija. Mifumko ya bei duniani, ripoti ilisisitiza, huchochewa, kwa kiasi, na bei kubwa ya mafuta iliojiri karibuni pamoja na bei ya juu ya bidhaa nyengine muhimu kwenye masoko ya kimataifa.

Kwa kukhitimisha, ripoti ya IMF ilithibitisha ya kuwa uchumi ulionyesha mzoroto wa kupigiwa mfano ulikuwa ni ule wa mataifa ya Marekani na Ulaya ya magharibi. Ama kuhusu uchumi wa Ujapani, ripoti iliendelea kusema, haukuathiriwa sana kama mataifa ya Ulaya na Marekani kutokana na mvutano kwenye soko la fedha. Kwa sababu uchumi wa Ujapani umejaaliwa vyanzo imara vyenye uwezo kinga wa kujirekibisha na kukabili mabadiliko kwa nguvu isiyoterereka. Uchumi wa mataifa yanayofufuka kimaendeleo, pamoja na zile nchi zinazoendelea, ripoti ilibainisha kuwa huko haikuathirika kwa sababu ya mgogoro wa fedha uliotukia nchi za maendeleo ya viwanda. Uchumi wa mataifa yanayoendelea, kwa ujumla, ripoti ilisisitiza, unazidi kukuwa kwa kasi, ukiongozwa na Uchina na Bara Hindi, ijapokuwa harakati hizo katika baadhi ya mataifa yanayoendelea zimeanza kupwelewa kidogo.