Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Djibouti inakurubia ukingo wa janga la njaa, WFP yaonya

Djibouti inakurubia ukingo wa janga la njaa, WFP yaonya

Dally Belgasami, Mkurugenzi wa Ofisi ya Geneva ya Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) aliwaarifu waandishi habari kwamba Djibouti ipo ukingoni mwa janga la njaa ya halaiki na inahitajia kufadhiliwa, kidharura, msaada wa chakula na wahisani wa kimataifa ili kunusuru umma na vifo.

Belgasami alizuru taifa hilo karibuni na alitahadharisha ya kwamba mzozo mkubwa wa chakula unaokabili Djibouti, ukichanganyika na kutanda kwa ukame na kupanda kwa kasi kwa bei za chakula ni mambo yanayowasukuma raia kwenye maafa ya njaa. Shirika la UM linalohudumia misaada ya chakula duniani, yaani WFP, linahitajia kupatiwa msaada wa dola milioni 19 sasa hivi kununua chakula cha kuwalisha raia dhaifu na mafakiri Djibouti [mnamo miezi 17 ijayo], pamoja na tani 17,000 ziada zinazohitajika kuendeleza shughuli zao nchini humo kuanzia sasa hadi Machi 2009. Djibouti ni taifa ambalo huagizishia asilimia 100 kamili ya chakula kutoka nje.