Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limekutana Ijumaa kuzingatai shughuli za Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) na pia kufanya mapitio ya ripoti ya KM kuhusu ombi la Nepal la kutaka UM usaidie kuimarisha mpango wa amani nchini humo. Baraza la Usalama limeamua kuongeza muda wa kazi kwa majaji wanaohusika na mauaji ya Rwanda, ili kuhakikisha kesi zilizosalia zinakamilishwa kwa muda unaotakiwa na ICTR.

Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) linafanya mapitio na kutathminia ripoti za mwaka kuhusu shughuli za mashirika ya UM na vitengo vyake kadha wa kadha viliopo sehemu mbalimbali za dunia, na baadaye kupitisha mapendekezo yanayofaa kutekelezwa kwenye shughuli za kazi.

Vikosi vya mchanganyiko vya UM/UA vinavyolinda amani Darfur (UNAMID) vilioongoza taadhima maalumu ya kumkumbuka mwanajeshi wa Nigeria, Meja Shehu Abdullahi Gada aliyeuawa na washambulizi wasiojulikana mnamo Julai 16 kwenye mji wa Forobaranga, Darfur Magharibi. Kamanda Mkuu wa UNAMID, pia kutoka Nigeria, aliwaambia waliohudhuria kumbukumbu za kumwaga marehemu kwenye mji wa El Fasher kwamba "wanafarajika na ukweli uliodhihiri kwao wote kwamba marehemu Gada alijitolea mhanga kuimarisha utu na ubinadamu, juu ya kuwa na umri mdogo."

Sweden imeteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa tume ya Kamisheni ya UM kuhusu Ujenzi wa Amani kuongoza juhudi za kuisaidia Burundi kufufua huduma za maendeleo ya kiuchumi na jamii na kuikinga na hatari ya kuteleza tena kwenye hali ya uhasama na mapigano.