Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Naibu KM wa UM Asha-Rose Migiro, kwenye risala alioitoa mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika unaofanyika Sharm el-Sheikh, Misri kuanzia Ijumatatu amepongeza uamuzi wa kuingizwa mada inayohusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwenye ajenda yao - hususan lile saula la kuyapatia mataifa yanayoendelea usafi wa mastakimu na maji salama.

KM wa UM amemteua Alain Le Roy wa Ufaransa kuwa KM Mdogo wa Idara ya UM kuhusu Operesheni za Ulinzi wa Amani (DPKO), na atachukua nafasi hiyo kutoka Jean-Marie Guehenno ambaye atamaliza muda wake wa kazi karibuni.

Kadhalika, KM Ban akishirikiana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wamemteua Djibril Yipene Bassole wa Burkina Faso kuwa Mpatanishi wa Pamoja wa UM/UA kwa Darfur; aanatazamiwa kuongoza shughuli zake kwa muda kamili kutokea ElFasher,Darfur na atapatiwa ushauri ziada, pindi utahitajika, kutoka kwa Wajumbe Maalumu kwa Darfur wa UM na UA, yaani Jan Eliasoon na Salim Ahmed Salim.

Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio liliofafanua kwa uwazi zaidi, kwa Mataifa Wanachama, tafsiri halisi juu ya namna ya kutekeleza vikwazo dhidi ya makundi, watu binafsi na pia vitengo vya kimataifa na kitaifa vilivyyohusiana na makundi ya al-Qaeda na Taliban, ikiwa miongoni mwa juhudi za kupiga vita ugaidi mamboleo.

Kuanzia tarehe mosi Julai Uraisi wa Baraza la Usalama utaongozwa na Vietnam baada ya taifa la Marekani kumaliza muda wake mwisho wa mwezi Juni.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limemteua Elia Armstrong wa Kanada kuwa mkuu mpya wa Ofisi ya Maadili ambapo atasimamia utekelezaji wa majukumu ya kikazi miongoni mwa watumishi wa taasisi hiyo.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limekadiria gharama ya uharibifu uliojiri mwezi uliopita kwenye sekta ya kilimo, katika jimbo la Sichuan, Uchina kufuatia zilzala iliopiga kieneo, ilikuwa ni sawa na dola bilioni 6; na watu milioni 30 waliopo vijijini ndio inasemekana walioathirika zaidi na kupoteza fungu kubwa la rasilmali zao.