Dereva wa WFP Sudan Kusini ameuawa kwa kuvizia
Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuuliwa dereva wao aliyeajiriwa kutoka Uganda, Muzamil Ramadan Sida mwenye umri wa miaka 28 ambaye alishambuliwa kwa kuvizia kwenye barabara ya Juba-Yei, Sudan kusini, baada ya kuteremsha shehena ya chakula kwenye ghala za WFP ziliopo Juba. Marehemu Sida ni dereva wa tano wa WFP kuuawa Sudan Kusini tangu mwanzo wa mwaka.
WFP imeitumia aila ya marehemu Sida mkono wa taazia.
Kadhalika WFP imetangaza kwamba imepokea msaada wa fedha wa karibu dola milioni 15 zinazohitajika kusaidia kupeleka misaada ya kiutu kwa kutumia ndege, hasa kwenye maeneo ambayo hayawezi kufikiwa kwa usafiri wa ardhini kwa sababu ya hatari zilizovuma barabarani za ujambazi na uharamia. Huduma hizi zitaendeshwa mpaka mwisho wa Septemba na kuwasaidia watumishi wanaowakilisha mashirika 200 ziada yaliopo Sudan kuendeleza shughuli zao.