Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupwelewa kwa udhibiti wa madawa haramu kunahatarisha usalama wa mataifa yanayoendelea, UM yaonya

Kupwelewa kwa udhibiti wa madawa haramu kunahatarisha usalama wa mataifa yanayoendelea, UM yaonya

Ofisi ya UM Kuhusu Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) Alkhamisi imewasilisha Ripoti ya 2008 juu ya Madawa Haramu Duniani ambayo ilionya kwamba maendeleo katika udhibiti wa matumizi ya madawa hayo yanahatarishwa na kukithiri kwa uzalishaji wa majani ya koka pamoja na mazao ya afyuni au kasumba ulimwenguni.

Ripoti ilisema kwamba tangu 2005 uzalishaji wa kasumba ulikithiri mara mbili zaidi katika Afghanistan, na asilimia 80 ya mazao haya maututi yalivunwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani wa serikali wa kundi la Taliban. Kadhalika katika taifa la Colombia, Amerika ya Kusini mavuno ya majani ya coka yaliongezeka kwa asilimia 27 mnamo 2007 kwenye yale maeneo yaliopo chini ya mamlaka ya waasi wanaopinga serikali. Mkuu wa Ofisi ya UNDOC amependekeza hatua za haraka zichukuliwe kwa pamoja na Mataifa Wanachama kudhibiti bora biashara haramu ya madawa ya kulevya, ambayo imeonekana katika siku za karibuni kuenea kwa wingi zaidi katika mataifa ya Afrika Magharibi.