Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mkutano wa Mapitio ya Mapatano ya Durban kufanyika mwakani Geneva

Baada ya mvutano wa majadiliano miongoni mwa wanadiplomasiya wa kimataifa, wanachama wa Kamati ya Matayarisho ya Mkutano wa Mapitio ya Mapatano ya Durban, waliokutana Geneva, Ijumatatu wamekubaliana kuitisha kikao hicho Geneva mwezi Aprili, 2009 ambapo wajumbe wa kimataifa wanatarajiwa kuzingatia hatua za kuchukuliwa, kukabiliana, kwa nguvu moja, na masuala sugu ya ubaguzi na chuki za wageni. Matatizo haya bado yanaendelea kusumbua umma wa kimataifa katika karne tuliomo hivi sasa.

Uchina unahitajia wahudumia afya, na maelfu ya mahema, kwa majeruhi wa zilzala

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti ya kuwa Serikali ya Uchina ipo tayari kupokea timu za wahudumia afya wa kimataifa, watakaotumiwa kusaidia raia waliosibiwa na zilzala katika jimbo la Sichuan. Kadhalika, Serikali imetoa ombi maalumu leye kupendekeza ifadhiliwe mahema milioni 3.3 na jamii ya kimataifa, kuwasaidia kupata makazi ya muda waathiriwa wa zilzala waliopoteza nyumba zao.

Aila zilizong'olewa makazi na mapigano Sudan zinapatiwa huduma za msingi na IOM

Msemaji wa Shirika la IOM, Jean Phillipe Chauzay, aliwaambia waandishi habari katika Makao ya Ofisi za UM-Geneva juu ya huduma zao zinavyotekelezwa kufarajia kidharura misaada ya kihali kwa makumi elfu ya watu waliokimbia mapigano makali yaliotukia siku za karibuni kwenye mji wa Abyei,Sudan, baina ya majeshi ya taifa ya Sudan (SAF) na kundi la SPLM. Mji wa Abyei ni eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na ni miongoni mwa zile sehemu za Sudan zenye kujulikana rasmi kama maeneo ya mpito, ambayo yanasubiri kupatiwa usuluhishi wa nani mwenye haki ya mamlaka.

UNHCR itachunguza hadhi ya sheria mpya Utaliana inayofananisha uhamiaji na jinai

Shirika la Wahamiaji la UNHCR limeripoti kuwa litafuatilia, kwa ukaribu na makini zaidi, maana hakika ya sheria mpya iliopitishwa Ijumatano kwenye Mji wa Naples na Baraza la Mawaziri Utaliana, inayothibitisha kitendo cha uhamiaji usio halali kuwa sawa na kosa la jinai na uhalifu, ambao utastahiki hukumu ya kifungo cha muda mrefu gerezani kwa mtuhumiwa. ~~Kwa mujibu wa sheria hii mpya watu ambao ombi lao la kupata hifadhi ya kisiasa limekataliwa watalazimika kuondoka Utaliana bila ya fursa ya kukata rufaa; na wale wanaotaka kuomba hifadhi, ambao mara nyingi huingia nchini kwa njia zisio rasmi, wao watashitakiwa kufabya kosa la jinai lenye hukumu ya kifungo cha angalau miaka minne.~~ ~

Ripoti juu ya hali ya kigeugeu ya wahamiaji wandani Kenya

Hivi karibuni UM ulipokea taarifa zenye kudai wenye mamlaka nchini Kenya wameanisha shughuli za kufunga zile kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi - au kwa lugha rasmi ya UM \'wahamiaji wa IDPs\' - ambao maelfu yao waling’olewa makwao baada ya kuzuka nchini machafuko na vurugu liliofuatilia matokeo ya uchaguzi mnamo mwisho wa 2007.

Baraza la HRC lazingatia mzozo wa chakula duniani

Baraza la Haki za Binadamu (HRC) Alkhamisi mjini Geneva lilifanyisha kikao maalumu, kusailia mzozo wa mifumko ya bei za chakula duniani. Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour kwenye hotuba yake ya ufunguzi altahadharisha kwamba bila ya, kwanza, kulitatua tatizo la chakula kwa suluhu ya jumla, na ya kuridhisha, itakayozingatia kihakika haki za ule umma maskini, uliotengwa na kudharauliwa kwenye jamii zao, kuna hatari zile juhudi zote za kuudhibiti mzozo huu kimataifa kwenda arijojo mathalan miporomoko ya vipande vya dhumna.