Upatanishi wa amani unahitajika kuimarisha uhusiano bora kati ya UM na UA, anasihi KM Ban
Baraza la Usalama Ijumatano lilikutana kwenye kikao maalumu, cha hadhi ya juu, kilichofanyika kwenye Makao Makuu mjini New York, kwa madhumuni ya kujadilia namna ya kuongeza ushirikiano halisi na ushikamano wa kuridhisha kati ya UM na taasisi zake, hasa ile taasisi ya Baraza la Usalama, pamoja na Umoja wa Afrika (UA), hususan kwenye juhudi za kuzuia na kutatua kwa amani migogoro iliolivaa bara la Afrika. Kwenye hotuba alioitoa KM Ban Ki-moon katika mkusanyiko wa Baraza la Usalama, alisistiza ya kuwa utaratibu unaochukuliwa na jumuiya ya kimataifa kusuluhisha fujo na mizozo iliopo Afrika, kwa njia za amani, ni lazima ukuzwe na upewe umuhimu wa hadhi ya juu na UM pamoja na Umoja wa Afrika.