Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upatanishi wa amani unahitajika kuimarisha uhusiano bora kati ya UM na UA, anasihi KM Ban

Upatanishi wa amani unahitajika kuimarisha uhusiano bora kati ya UM na UA, anasihi KM Ban

Baraza la Usalama Ijumatano lilikutana kwenye kikao maalumu, cha hadhi ya juu, kilichofanyika kwenye Makao Makuu mjini New York, kwa madhumuni ya kujadilia namna ya kuongeza ushirikiano halisi na ushikamano wa kuridhisha kati ya UM na taasisi zake, hasa ile taasisi ya Baraza la Usalama, pamoja na Umoja wa Afrika (UA), hususan kwenye juhudi za kuzuia na kutatua kwa amani migogoro iliolivaa bara la Afrika. Kwenye hotuba alioitoa KM Ban Ki-moon katika mkusanyiko wa Baraza la Usalama, alisistiza ya kuwa utaratibu unaochukuliwa na jumuiya ya kimataifa kusuluhisha fujo na mizozo iliopo Afrika, kwa njia za amani, ni lazima ukuzwe na upewe umuhimu wa hadhi ya juu na UM pamoja na Umoja wa Afrika.

Kwa kuambatana na hayo ndipo KM Ban alipobainisha kwenye risala aliowasilisha mbele ya Baraza la Usalama kwamba hivi sasa ameingiwa wasiwasi juu ya kuzorota kwa hali ya kigeugeu iliyotanda Zimbabwe, ambapo matokeo ya uchaguzi wa uraisi uliofanyika Machi 29 yamecheleweshwa kutangazwa, wakati raia wanatangatanga kutaka kuchukuliwe hatua za dharura ili kuharakisha uamuzi usio na shaka wa matokeo ya uchaguzi, utakaoridhia wote. Kabla ya Baraza la Usalama kukamilisha majadiliano kulipitishwa, kwa kauli moja, azimio liliotoa mwito unaohimiza kuchukuliwa hatua madhubuti za kuimarisha uhusiano bora baina ya UM na mashirika ya kikanda, ikijumuisha Umoja wa Afrika, kwenye masuala ya usalama na amani.