Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UNHCR imesitisha misaada katika JKK baada mapigano kufumka

Ron Redmond, Msemaji wa Shirika la UNHCR aliwaambia waandishi habari Ijumaa mjini Geneva kwamba shirika lao limelazimika kusitisha ugawaji wa misaada ya kihali kwa wahamaji wa ndani ya nchi waliopo Jimbo la Kivu Kaskazini, katika JKK, baada ya kuzuka tena mapigano mapya katika eneo hilo. Hata hivyo, UNHCR bado inaendelea kuisaidia Serikali ya JKK kusajili wahamaji wanaomiminikia katika eneo la Rutshuru liliopo kilomita 70 kaskazini ya mji wa Goma. Idadi ya wahamaji wa ndani ya nchi waliopo Kivu Kaskazini kwa hivi sasa inakadiriwa 860,000.

Ukosefu wa nishati wailazimisha UNRWA kusitisha misaada Ghaza

Shirika la UM linalosimamia Huduma za Kiutu katika Maeneo ya Wahamiaji wa Kifalastina Mashariki ya Kati, UNRWA, limeripoti na kuthibitisha kwamba limesitisha kupeleka chakula kwa umma muhitaji waliopo kwenye Tarafa ya Ghaza, kwa sababu ya ukosefu wa petroli inayohitajika kutumiwa kwenye malori yanayotumiwa kugawa misaada hiyo.

UNICEF inaonya, bei kubwa ya chakula inahatarisha maisha ya watoto

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti kuwa na wasiwasi kuhusu uhaba wa lishe kwa wanawake na watoto wa mataifa yanayoendelea, kwa sababu ya muongezeko mkubwa wa bei za chakula duniani katika kipindi cha karibuni. UNICEF inakhofia tatizo la kupanda kwa kasi kwa bei ya chakula duniani, kunachochea na kukithirisha athari mbaya za kiuchumi na kijamii katika mataifa masikini, ambapo kabla ya mgogoro huo kuzuka familia hizo zilikuwa zikitumia asilimia 70 ya pato lao kununua chakula, na inakhofiwa hizi ndio jamii zitakazoumizwa na kudhurika zaidi na kupanda kwa bei ya chakula katika soko la kimataifa.

ILO inasema udhibiti bora makazini huokoa maisha

Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) limetoa ripoti mpya yenye kuonyesha watu milioni 2.2 hufariki kila mwaka katika dunia kwa sababu ya ajali zinazoambatana na ajira pamoja na maradhi wanayopata makazini. ILO imependekeza taratibu za usimamizi kwenye mahali pa kazi zirekibishwe ili kuwawezesha viongozi na mameneja kutambua na kubashiria mapema zaidi hatari ziliopo na kuzidhibiti mapema kabla hazijasababisha vifo vya ajali.

UM inawakumbuka watumishi waliofariki wakihudumia bodi la kimataifa

Tarehe ya leo Aprili 25 inaheshimiwa hapa Makao Makuu kama Siku Maalumu ya Kuwakumbuka Wafanyakazi wa UM waliopoteza maisha wakati wakitumikia taasisi hiyo ya walimwengu. Katika taadhima zilizofanyika kwenye bustani ya Makao Makuu, waandishi habari wenziwetu kutoka Redio ya UM, Geraldine Adams na Jerome Longue walisoma orodha ya majina ya wafanyakazi 294 waliofariki tangu Disemba 2005.

Mjumbe wa Afrika Mashariki kwenye UNCTAD XII asailia kikao

Wajumbe kadha kutoka Mataifa Wanachama wa UM walikusanyika katika mji mkuu wa Accra, Ghana kuhudhuria kikao cha 12 cha Taasisi ya UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ambacho kilifunguliwa rasmi Aprili 20, na mijadiliano yaliendelea karibu wiki moja. Mkutano Mkuu wa UNCTAD hufanyika kila baada ya miaka minne. Dhamira ya kikao cha mwaka huu cha 12 ilikuwa kuzingatia taathira zinazoletwa na huduma za msawazisho wa lazima wa shughuli za uchumi katika soko la kimataifa, au kwa lugha nyengine kuzingatia taathira ya marekibisho yaliochochewa na mfumo wa utandawazi.

UM kuiadhimisha rasmi Siku ya Malaria Duniani

Kikao cha 60 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani (WHO), kilichofanyika Geneva mwezi Mei 2007, kilipitisha, kwa kauli moja pendekezo la kuifanya tarehe 25 Aprili kila mwaka iadhimishwe kuwa ni Siku ya Malaria Duniani. Makusudio ya pendekezo hili ni kuitumia siku hiyo kupigia mbiu ya mgambo zile juhudi za kimataifa za kudhibiti bora ugonjwa maututi wa malaria. ~

Operesheni za amani mipakani Ethiopia/Eritrea zatathminiwa upya na BU

Wajumbe wa Baraza la Usalama walikutana kwenye kikao cha faragha, mapema wiki hii, kwa muda wa saa tatu, kushauriana juu ya marekibisho yanayotakikana kuchukuliwa na jumuiya ya kimataifa kuhusu shughuli za vikosi vya UNMEE vinvyohudumia ulinzi wa amani mipakani Ethiopia na Eritrea. Wajumbe wa kimataifa katika Baraza la Usalama wamependekeza kuitishwe kikao chengine wiki ijayo kufuatilia mazungumzo magumu ya kuamua kama UM uendelee kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kusitisha mapigano mipakani kati ya Ethiopia na Eritrea au la.