Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UNHCR imesafirisha Kenya misaada ziada ya kiutu

Mnamo mwisho wa wiki iliopita, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) lilipeleka nchini Kenya mahema 2,345 yatakayotumiwa na makumi elfu ya zile familia zilizong’olewa makwao baada ya machafuko kufumka nchini mwanzo wa mwaka kufuatia uchaguzi.

Mkuu wa OCHA anasihi, 'suluhu za dharura na muda mrefu zahitajika Kenya'

Ijumatatu Mshauri wa KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes aliripoti kwa Baraza la Usalama juu ya ziara yake ya karibuni katika Kenya. Aliwaambia wajumbe wa Baraza kwamba bila ya kupatikana suluhu ya haraka juu ya masuala ya kisiasa nchini, kuna hatari ya vurugu kufufuka upya na kukithirisha mfarakano wa kijamii. Holmes alizipongeza juhudi za KM Mstaafu Kofi Annan za kuleta suluhu ya kuridhisha ya kisiasa. Kadhalika, alisisitiza kwamba wahamaiji wa ndani ya nchi (IDPs) walioathirika na machafuko ya karibuni wataendelea kutegemea wahisani wa kimataifa kuwafadhilia misaada ya kiutu kwa, angalau, mwaka mmoja.

Hapa na pale

Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Masuala ya Mgogoro na waasi wa LRA Uganda Kaskazini, Joaquin Chissano, Raisi wa zamani wa Msumbiji, amenakiliwa kuripoti kupatikana maafikiano ya kutia moyo mwisho wa wiki, baada ya Serikali ya Uganda na waasi wa LRA walipotiliana sahihi kwenye mji wa Juba, Sudan Kusini, mwafaka wa kudumisha kuacha kupigana.~

KM ameanzisha rasmi kampeni ya kimataifa dhidi ya unyanyasaji wa wanawake

Asubuhi ya leo, Ijumatatu, Februari 25, KM wa UM Ban Ki-moon alianzisha rasmi kampeni ya kimataifa ya kukomesha na kufyeka tabia ya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya wanawake na watoto wa kike duniani. Kampeni ilitilia mkazo umuhimu na ulazima wa kukomesha kidharura vitendo vyote vya udhalilishaji wa kijinsia. Kampeni hii imeanzishwa siku ile ile ambapo Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW)ilipfungua rasmi, kwenye Makao Makuu ya UM, kikao cha mwaka, cha 52. Tutakupatieni taarifa zaidi juu ya Mkutano wa CSW hapo kesho. ~

Usalama wa raia Darfur Magharibi unatia kiherehere

Ijumapili Mshauri wa UM juu ya Misaada ya Kiutu katika Sudan, Ameerah Haq pamoja na Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa Ubia wa UM/UA na pia Mkuu wa Vikosi Mseto kwa Darfur (UNAMID) walitoa risala iliobainisha kuingiwa na ‘khofu kuu’ juu ya usalama wa maelfu ya raia wanaoishi katika sehemu ya Jebel Muun, Darfur Magharibi kutokana na hujuma za karibuni kwenye maeneo yao.

OHCHR inalaani ukiukaji wa haki za binadamu Chad

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki Binadamu (OHCHR) imearifu kupokea taarifa za kutia wasiwasi zilizoonyesha vikosi vya usalama vya Serikali viliwateka nyara viongozi kadha wa upinzani, pamoja na kuwashika viongozi wa jumuiya za kiraia na kuwatia kizuizini baada ya kutukia mashambulio ya waasi karibuni kwenye mji mkuu wa N’Djamena, Chad .

Hapa na pale

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa ulimwengu unakabiliwa na ukosefu wa wahudumia afya milioni 4, na eneo lenye upungufu mkubwa zaidi ni bara la Afrika ambalo pekee linahitajia kidharura wafanyakazi milioni moja ziada ili kuweza kuyafikia malengo ya maendeleo na afya bora kama ilivyodhamiriwa na Nchi Wanachama. Kuanzia tarehe 2 hadi 7 Machi jumuiya ya kimataifa itakusanyika mjini Kampala, Uganda kuhudhuria mkutano wa kimataifa utakaojumuisha wataalamu wa serikali, wale wa kutoka sekta ya afya, vyuo vikuu na pia mashirika yasio ya kiserekali, ili kuzingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kusuluhisha tatizo la upungufu wa wahudumia afya duniani.

'Fujo na ghasia za makundi ni mutlaki' kuonya Mjumbe wa UM Liberia

Ellen Margrethe Loj, Mjumbe Maalumu wa UM katika Liberia alipokutana Alkhamisi na raia waliohudhuria mkutano wa hadhara katika mji wa Tappita, wilaya ya Nimba nchini Liberia, alitoa nasaha kali iliyowaonya kujiepusha na tabia karaha ya makundi kutumia nguvu na fujo na kuchuka haki mikononi mwao.Alisema tabia hii inatengua sheria za kitaifa na kimataifa.

UM wasaidia kuwapatia watoto wa Cameroon chanjo kinga

UM ikishirikiana na Serikali ya Cameroon pamoja na zile jumuiya zisio za kiserekali zimefanikiwa kukamilisha huduma ya kuwachanja watoto 35,000 dhidi ya shurua na maradhi ya kupooza/polio katika wilaya ya Koussei, kaskazini-mashariki ya Cameroon. Asilimia kubwa ya watoto hawa walikuwa ni raia wa Chad waliohamia Cameroon baada ya machafuko kufumka kwenye mji mkuu wa N’Djamena, Chad.