Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinzi Amani wa UNMEE wazuiliwa na Eritrea kwenda Ethiopia

Walinzi Amani wa UNMEE wazuiliwa na Eritrea kwenda Ethiopia

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani Mipakani Ethiopia na Eritrea (UNMEE) limeripoti kwamba wenye madaraka katika Eritrea bado wanaendelea kuzuia wanajeshi pamoja wafanyakazi wa kiraia wa UNMEE kuvuka mpaka kwenda uhamishoni wa muda nchini Ethiopia.

Balozi Ricardo Alberto Arias wa Panama, aliye Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Februari aliwaambia waandishi habari baada ya mashauriano kumalizika kwamba Mataifa yote 15 Wanachama "yamelaani kipamoja hatua ya Eritrea kutojali mapendekezo ya Baraza la Usalama."

Mnamo mwanzo wa Februari UM uliamua kuwapeleka kwenye uhamisho wa muda Ethiopia wafanyakazi na walinzi wa amani wa lile Shirika la UNMEE baada ya Eritrea kulinyima nishati za dizeli inayohitajika kuhudumia shughuli zake mipakani. Kadhalika akiba ya chakula ya UNMEE ilianza kupungua kwa kasi baada ya ya kuarifiwa na kampuni iliyokuwa ikihudumia chakula kwamba haitoweza tena kuwatekelezea mahitaji hayo.