Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA anasihi, 'suluhu za dharura na muda mrefu zahitajika Kenya'

Mkuu wa OCHA anasihi, 'suluhu za dharura na muda mrefu zahitajika Kenya'

Ijumatatu Mshauri wa KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes aliripoti kwa Baraza la Usalama juu ya ziara yake ya karibuni katika Kenya. Aliwaambia wajumbe wa Baraza kwamba bila ya kupatikana suluhu ya haraka juu ya masuala ya kisiasa nchini, kuna hatari ya vurugu kufufuka upya na kukithirisha mfarakano wa kijamii. Holmes alizipongeza juhudi za KM Mstaafu Kofi Annan za kuleta suluhu ya kuridhisha ya kisiasa. Kadhalika, alisisitiza kwamba wahamaiji wa ndani ya nchi (IDPs) walioathirika na machafuko ya karibuni wataendelea kutegemea wahisani wa kimataifa kuwafadhilia misaada ya kiutu kwa, angalau, mwaka mmoja.

Alionya ya kwamba hata kungelipatikana suluhu ya mapema kuhusu matatizo ya kisiasa yaliolivaa Kenya, bado kutahitajika kuzingatiwa kihakika yale masuala yenye utata ambayo mizizi yake imeselelea kwa muda mrefu kwenye mfumo wa jamii Kenya. Masuala haya, aliongeza kusema, hufungamana na tatizo la umilikaji wa ardhi pamoja na kusambaa kwa mazingira ya hali duni na tofauti za kiuchumi na za kimatabaka zilizodhihiri miongoni mwa raia. Halkadhalika, alisisitiza, suala la uwakilishi katika shughuli za serikali ni tatizo lenye kuamsha hisia aiana kwa aina. Alinansihi kwamba utatuzi wa masuala haya utahitajia mchango mkubwa wa wanasiasa wote wa Kenya, wakisaidiwa na jamii ya kimataifa, halkadhalika. Alimaliza kwa kuahidi UM utaendelea kuisaidia Kenya kwa kila njia kukabiliana vilivyo na matatizo hayo, na itajitahidi kuimarisha misaada yake ya kiutu kwa umma muhitaji nchini humo na kukuza huduma za maendeleo mnamo miezi ijayo.