Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Neno La Wiki

Neno la Wiki-Kipakatalishi

Mchambuaji wetu leo ni Nuhu Zuberi Bakari, Naibu mwenyekiti wa maswala ya mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya CHAKITA. na anatufafanulia maana ya neno Kipakatalishi, neno ambalo anasema yeye amelitunga na likakubalika Afrika ya Mashariki na Kati.

Neno Kipakatalishi kinamaanisha Laptop ambacho ni chombo kinachotumia vitarakilishi, kwa sababu inatumia tarakimu na maandishi na pia hupakatwa.

Neno la wiki-papa

Katika Neno la Wiki hii  Ijumaa Juni 10 tunaangazia neno papa na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Utandawazi au Utandaridhi?

Katika neno la wiki tunachambua maneno utandawazi na utandaridhi, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Maneno haya yote yako kwenye kiswahili lakini ni lipi sahihi kutumia?.

Nuhu Zuberi Bakari anazungumzia matumizi ya maneno haya hususan Kenya na Tanzania.  Anasema maneno haya yanatumika kwa maana sawa lakini utofauti unaibuka kwa sababu ya mazingira yanakotumika.

Neno la Wiki- Kandelinya

Katika Neno la Wiki hii  tunaangazia neno Kandelinya na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Onni Sigalla anazungumzia matumizi ya neno Kandelinya. Anasema Kandelinya ni birika mahususi kwa ajili ya kutengenezea chai au maji, na pia linaweza kuwa ni birika maalum kwa ajili ya kuoshea mikono kabla na baada ya kula. Kandelinya pia  ni aina ya muhogo ambao ni mchungu na huliwa tu baada ya kuuvundika na kukaushwa kwa ajili ya kutengenezea makopa.

Neno la wiki-limbukeni

Ijumaa ya tarehe 16 Mei mwaka 2016 tuliangazia matumizi ya neno limbukeni. Mtaalamu wetu alikuwa Onni Sigalla, mhariri mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.
Bwana Sigalla anaangazia neno limbukeni ambapo anafafanua limbukeni kama mtu ambaye anapata kitu kwa mara ya kwanza aghalabu kitu chenye thamani na kuonyesha kukiajabia sana.

Sifuri ama Sufuri, ni lipi?

Katika neno la wiki tunachambua neno Sufuri na Sifuri, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Maneno haya yote yako kwenye kiswahili lakini ni lipi sahihi kutumia?.

Nuhu Zuberi Bakari anazungumzia matumizi ya maneno haya hususan Kenya na Tanzania.  Anasema Sifuri hutumika Tanzania na Sufuri Kenya, na yote ni sawa, lakini kwa maoni yake anasema Sifuri ndio sahihi zaidi.

Neno la wiki- Mazishi au maziko?

Ijumaa ya tarehe 29 Mei mwaka 2016 tuliangazia matumizi ya maneno maziko na mazishi. Mtaalamu wetu alikuwa Onni Sigalla, mhariri mwandamizi,  Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Bwana Sigalla, mazishi huanza pale mtu anapokata roho au kufariki dunia, shughuli zote kama zile watu kukusanyika na kupeana taarifa mbali mbali ikiwemo kuchangishana, hayo ni mazishi na hayapangiwi muda.